MAPAMBANO kati ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kiteto
mkoani Manyara, yanaendelea kushika kasi na kusababisha watu wanne
kupoteza maisha.
Hali hiyo ilibainishwa na Katibu wa wakulima wilayani hapa, Josephat
Mponda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wilayani.
Mponda alisema kuwa usiku wa kuamkia juzi, jamii ya wafugaji wa
Kimasai waliwavamia wakulima katika eneo la Lepono na kusababisha
mkulima mmoja na wafugaji watatu kupoteza maisha.
Mponda alieleza kuwa kati ya majira ya saa saba na nane usiku, jamii
ya wafugaji wa Kimasai waliwavamia wakulima kwa kutumia silaha za moto
jambo ambalo lilizua mashambulizi kati ya pande mbili na kusababisha
vifo vyawatu hao.
Katibu huyo alisema jamii hiyo ya wafugaji ilivamia maeneo ya Laitini
na kuvichoma moto vibanda vya wakulima jambo ambalo lilizua mapambano
makali kwa jamii hiyo.
“Kinachoshangaza ni kuwa jamii ya Kimasai inatumia silaha kubwa na
nzito huku wakiwa wanajitamba kuwa wanazipata kutoka kwa viongozi na
kueleza kuwa watahakikisha wakulima wanaondoka katika maeneo haya ili
wabaki wafugaji pekee.
“Lakini cha kushangaza ni Jeshi la Polisi kutokuwa na ukweli katika
utoaji wa taarifa kwa wakuu wao wa kazi. Mfano katika mauaji haya
yaliyotokea askari wamechukua maiti moja na kuipeleka katika hosptiali
ya Kiteto, maiti nyingine tatu wameziacha porini jambo ambalo
linaonekana kuficha ukweli wa mambo na kusababisha machafuko kuendelea
kuwa makubwa,” alieleza Mponda.
Alisema kuwa iwapo serikali itashindwa kutatua mgogoro huo ambao kwa
sasa umechukua miaka mingi, ni wazi kutafikia hatua ya wakulima na
wafugaji kuanza vita na Kiteto hakutakalika.
Mkuu wa Polisi Mkoa wa Manyara, Mkilimali Mpwapwa alisema taarifa za
awali alizozipata kutoka kwa OCD wa Kiteto ni kuwa mkulima mmoja
amefariki na watu watatu wamejeruhiwa.
“Taarifa za awali nilizozipata kutoka kwa OCD ni kuwa mtu mmoja
ambaye ni jamii ya wakulima amepoteza maisha na watu wengine watatu
wamejeruhiwa na kati ya hao wakulima ni wawili na mfugaji ni mmoja.
“Imeelezwa kuwa walioanza kuvamia wenzao ni wafugaji kwa kuwavamia
wakulima na ndipo walipoanza kujibishana kwa kutumia silaha za kijadi
na kusababisha matukio ya mauaji kama hayo na hiyo ilitokea usiku wa
kuamkia Jumamosi,” alisema.
RPC Mpwapwa alisema taarifa hizo ambazo amezipata kutoka kwa OCD wake
zilikuwa bado hazijawa katika maandishi kutokana na kuendelea kufanya
uchunguzi wa matukio hayo.
“Kwakweli matukio ya Kiteto ni ya muda mrefu na yanatakiwa kutatuliwa
kwa njia ya kidiplomasia, vinginevyo kunaweza kutokea machafuko
makubwa kuliko yaliyopo kwa sasa, kwani ni juzi tu tulikaa na jamii zote
za wakulima na wafugaji na tukaongea nao na tukaamini kuwa mambo
yamekuwa shwari, lakini cha kushangaza kesho yake ndiyo yanajitokeza
mambo kama hayo, jambo hilo ni hatari sana na linaumiza vichwa vyetu,”
alisema RPC Mpwapwa.
Alisema mgogoro huo una vyanzo vingi vinavyochochea japo hakuvitaja,
lakini kauli hiyo inaweza kuhusishwa na matamko ya Naibu Spika wa Bunge
na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai ambaye alidai kuwa mgogoro huo
unakuzwa na ubaguzi wa viongozi pamoja na kuwepo kwa vitendo vya rushwa
kwa viongozi hao.
Katika mkutano wa hadhara kati yake na wakulima wa Kiteto, Chemba na
Kongwa, Ndugai alisema kuwa mgogoro huo unachangiwa na Mbunge wa Kiteto
na Naibu Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Benedict Ole-Nangoro
kwa kuonyesha wazi ubaguzi wa kikabila kati ya wakulima na wafugaji.
Mbali na hilo, Ndugai aliwataja Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema
Nchimbi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuwa ni kati ya viongozi aliodai
wanapokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kusababisha uamuzi kuwaelemea
wakulima ili waondolewe.
Desemba mwaka jana, jamii ya wakulima wapatao wanne walipoteza maisha
kutokana na mapigano yaliyozuka kati ya wakulima na wafugaji katika
kitongoji cha Olupoponyi anakotokea mbunge Ole-Nangoro.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment