Home » » TANI 7,400 ZA MAHINDI ZAKOSA SOKO

TANI 7,400 ZA MAHINDI ZAKOSA SOKO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wakulima wa Kijiji cha Galapo Wilayani Babati wakipakia mahindi yao kwenye magunia kwenye soko la Galapo Mkoani Manyara, jana.  

Zaidi ya tani 7,400 za zao la mahindi zilizozalishwa na wakulima wadogo wa kata za Galapo na Qash wilayani Babati mkoani Manyara zimekosa soko na kurundikwa katika Soko la Galapo, eneo ambalo zinaweza kuharibika wakati wowote.
Wakizungumza jana na mratibu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima wa Manyara (Mviwata), Martin Pius alisema wakulima hao waliiomba Serikali kufanya jitihada za haraka kwa kununua mahindi hayo ili kunusuru hasara kwa wakulima wa eneo hilo.
Mkulima wa Kijiji cha Galapo, Dodo Ekwani alisema wakulima wanateseka kwa kukosa fedha za kuwalipia ada watoto wao, kupata huduma za afya na pia kulipa vibarua na wakikosa viongozi wa kuwatetea juu ya hilo.
Mwenyekiti wa soko hilo, Lohay Langai alisema wakulima wa vijiji vya Galapo, Gedamary, Qash na Halu walileta mahindi yao sokoni wakitegemea Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula nchini (NFRA) wangenunua, lakini hali imekuwa tofauti.
Diwani wa Kata ya Galapo, Michael Naas Dil alisema suala hilo limekuwa kero katika kata yake na inampa wakati mgumu akiwa sehemu ya uongozi, hivyo ameiomba Serikali itoe fedha haraka kwa NFRA ili waweze kununua mazao hayo.
Mratibu wa Mviwata wa mkoa huo, Pius alisema soko ni suala muhimu na kichocheo kikubwa kwa uzalishaji na ubora wa mazao ya kilimo na inaweza kuwafanya wakulima wazalishe mazao mengi na kwa ubora unaohitajika.
“Hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilisaini mkataba na Kenya ili kununua mahindi ya wakulima, hivyo mchakato huo ufanywe haraka na taarifa ziwekwe wazi ili wakulima wadogo wafaidike,” alisema Pius.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa