Home » » UZAZI: WANAWAKE WAZALISHWA KWA KUTUMIA MIFUKO YA PLASTIKI MKOANI MANYARA

UZAZI: WANAWAKE WAZALISHWA KWA KUTUMIA MIFUKO YA PLASTIKI MKOANI MANYARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mzazi (kulia) akiwa wodini baada ya kujifungua
Baadhi ya wananchi na viongozi wao wanatetea nafasi ya wakunga kusaidia wajawazito kujifungua mkoani Manyara na wapo wataalamu wa afya ambao wanawatizama wakunga kama kundi lisilohitajika katika mchakato mzima wa afya ya mama na mtoto.

Wakati pande hizi mbili zikiendelea kuvutana, viongozi wa Serikali hadi sasa ni kama hawana msimamo wa moja kwa moja kuhusu suala hili, licha ya kuonekana kushangazwa na taarifa kwamba wapo wanaotumia mifuko ya plastiki (rambo au malboro) kwa ajili ya kuwasaidia wajawazito kujifungua.
Inakuwa kama jambo la kufikirika, lakini wapo wanawake wanaotoa ushuhuda kwani wao wamesaidiwa na wakunga wa jadi kwa kutumia mifuko ya plastiki kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali, ukiwamo Ukimwi na watoto wao hadi leo wanaishi wakiwa wenye afya na siha njema.
Margalena Saitoti ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ndirgish anasema yeye ni miongoni mwa wanawake waliosaidiwa kujifungua kwa kutumia mifuko ya plastiki, kutokana na wakunga wa jadi kutokuwa na mipira ya kuvaa mikononi ambayo hupatikana katika Kituo cha Afya cha Engusero.
“Mume wangu anafanya kazi ya ulinzi mjiniArusha, hivyo nikaona kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni bora wakunga hao wavae mifuko ya malboro mkononi, kwani wengine huwa na hofu kwamba vijana wanaotoka hapa kijijini na kwenda mijini huwa wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa Ukimwi,” anasema Saitoti.
Shuhuda mwingine ni Angela Moringe (25) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ndedo ambaye anasema watoto wake watatu wote alijifungua kwa wakunga wa jadi waliokuwa wanavaa mifuko ya plastiki kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali.
“Huku umasaini tumezoea kuzalishwa na wakunga wa jadi wakiwa wamevaa malboro na tunajifungua vizuri tu, kwasababu wakati wa ujauzito wanaume wetu wanatulazimisha kula vyakula ambavyo haviwezi kumnenepesha mtoto akiwa tumboni,” anasema Moringe.
Mkazi wa Kijiji cha Partimbo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa maelezo kwamba atakuwa akidhalilika, anasema wanawake wengi wana imani kubwa kwa wakunga wa jadi ndiyo maana wanakubali wazalishwe kwa kutumia mifuko ya plastiki kwani ni moja ya njia za kuepuka maambukizi ya Ukimwi.
“Kwa sababu hakuna mipira ya kuvaa mikononi, inawalazimu wavae mifuko ya plastiki japokuwa inakuwa inatuumiza wakati wa kupokea mtoto au wakati wa kusukuma, ila hatuna ujanja inabidi tukubaliane na hali halisi ilivyo,” anasema mwanamama huyo.
Kushamiri na kuaminika kwa wakunga wa jadi kunatokana na uchache wa vituo vya huduma za afya na tiba katika Wilaya ya Kiteto, hali inayochangia wanawake wengi wajawazito kujifungua wakiwa nyumbani.
Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto wilayani humo, Helena Batroba anasema mwaka 2012 ni wajawazito 2,818 tu sawa na asilimia 28 ya waliokuwapo wakati huo ndiyo waliojifungulia hospitalini, wakati wajawazito 7,196 sawa na asilimia 72 walijifungulia nyumbani.
“Kwa upande wa vifo vya wanawake wajawazito kwa mwaka jana vilikuwa vinne ambavyo vilitokea hospitalini na wanawake wajawazito wawili waliojifungulia nyumbani walifariki dunia,” anasema Batroba na kuongeza:
“Vifo 51 kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano vilitokea na vifo vya watoto wachanga wa hadi siku 28 hospitalini vilitokea 13 na nyumbani hakukuwa na taarifa za kifo chochote.”
Hoja za wataalamu
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Dk Leadry Malisa anasema wakunga wa jadi hawapaswi kuzalisha wanawake kwani linapotokea tatizo kwa mama mjamzito au kwa mtoto aliyezaliwa, hawawezi kutoa huduma stahiki zaidi ya kushuhudia kifo kati ya mzazi au mtoto.
“Unakuta kuna wakunga wengi wa jadi wanatumia mikono mitupu bila kuvaa mipira (gloves) kufanya kazi hizo huko nyumbani, bila kutambua kuwa wanajiweka kwenye hatari ya kupata magonjwa mbalimbali ikiwamo maambukizi ya virusi vya Ukimwi, wakati wa kuzalisha,” anasema Dk Malisa.
“Pia kutokuvaa ‘gloves’ mikononi wakati wa kuzalisha unaweza kupata maambukizi ya virusi vya hepatet (ugonjwa wa ini) ambao ni mbaya zaidi tofauti na maambukizi ya VVU, maambukizi ya magonjwa mengine au vyote kwa pamoja.”
Anasema changamoto ya upungufu wa vifaa vya kujifungulia ni tatizo ambalo  linakabili maeneo mengi hapa nchini na siyo wilayani Kiteto peke yake,  hivyo jamii inapoambiwa ichangie kuhusu kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kugharimia vifaa vya kujifungulia siyo tatizo.
Kwa upande wake, mratibu wa afya ya uzazi na mtoto wilayani Kiteto, Batroba, anasema wakunga wa jadi hawatakiwi kuzalisha wajawazito nyumbani kwani wamepewa mwongozo kupitia sera ya taifa ya afya inayowataka wanawake wajawazito kujifungulia kwenye huduma za afya.
Uongozi wa halmashauri
Hoja za wataalamu hawa zinapingwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mainge Lemalali ambaye anasema hakuna mtaalamu wa Idara ya Afya anayeweza kuwanyima wakunga wa jadi vifaa vya kujifungulia, ila tatizo ni upungufu wake.
 Lemalali anasema tatizo jingine ni uchache wa miundombinu ya afya hali inayowafanya wanawake wengi wa eneo hilo kushindwa kwenda hospitalini, wakati wa kujifungua kutokana na umbali uliopo kutoka katika makazi zilipo huduma za afya.

“Hili suala la wakunga wa jadi kutumia mifuko ya rambo kuvaa mikononi na kuzalisha nililisikia kwa mganga mkuu wa wilaya wakati tukiwa kwenye kikao cha kamati ya fedha, uongozi na mipango na mganga mkuu alikiri kabisa kwamba jambo hilo lipo na alishauri kwamba tuongeze bajeti ili wapatiwe mipira ya kuvaa mikononi, kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya VVU,” anasema Lemalali na kuongeza;
“Wakunga wa jadi ni watu muhimu kwenye wilaya yetu na sisi kama Serikali tunatambua mchango wao kwani amekuwa msaada mkubwa kwa jamii ambayo imekuwa ikishindwa kupata huduma za afya ikiwemo kujifungua kutokana na umbali mrefu wa vijiji vyao hadi katika zahanati, vituo  vya afya na hospitali.”
Anasema uhaba wa dawa bado ni tatizo na kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kiteto huwa na idadi kubwa ya wagonjwa, kwani baadhi yao wanatoka Wilaya za Kondoa na Chemba za Mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Kilindi ya mkoani Tanga.
RC anena
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo anapoulizwa kuhusu suala hili anashangazwa na matumizi ya mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuvaa mikononi na kuzalisha wanawake, badala ya mipira ya kitaalamu (gloves), huku akisema hajawahi kusikia jambo hilo.
“Wanatumia mifuko ya malboro kwa ajili ya kuzalisha! Watakuwa wanawaumiza wanawake wakati wa kujifungua, hilo suala ndiyo kwanza nalisikia kutoka kwako, silitambui kwa kweli kama kuna hayo unayonieleza,” anasema Mbwilo.
 Anasema inatakiwa elimu itolewe kwa wanawake hao kuwa wanapaswa kujifungulia kwenye huduma stahili hospitalini, kuliko nyumbani kwao kwani wanahatarisha maisha yao endapo ikitokea tatizo wakati wa kujifungua.


“Mfano mama huyu anapojifungua nyumbani ghafla mtoto anatanguliza miguu badala ya kichwa atafanyaje kama siyo kuhatarisha maisha yake na maisha ya mtoto pia, lazima wabadilike kwa kufuata huduma hiyo kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali,” anasema Mbwilo. Hata hivyo, anasema siyo vibaya halmashauri za wilaya kuwapa vifaa wakunga wa jadi wakati wa maandalizi wakiwa wajawazito kabla ya wanawake hao hawajajifungua kwani kuna baadhi ya wilaya huwa zinafanya jambo hilo.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa