Home » » Urais CCM, hofu ya uasi yatanda

Urais CCM, hofu ya uasi yatanda

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MAKUNDI ya wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), yanadaiwa kuanza mchakato wa kuhakikisha mgombea wanayemuunga mkono, ndiye anayeteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya chama katika Uchaguzi Mkuu.

Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, kundi la mgombea anayetajwa kutaka kuwania nafasi hiyo, limeanza kutumia kiasi
kikubwa cha fedha na kuzigawa kwa baadhi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), ambapo kitendo hicho kimefananishwa na uasi ndani ya chama.

Pia chanzo hicho kilisema baadhi ya wajumbe wa NEC wameanza kupewa maelekezo ya kufanya uasi dhidi ya vikao vya maamuzi ambavyo vitavyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.

Inadaiwa kuwa, hivi karibuni rafiki wa karibu na mgombea huyo, alipokea fedha kutoka nje ya nchi ili kufanikisha kampeni
ya mgombea wao kwa kuwaita baadhi ya wajumbe wa NEC nyumbani kwake na kuwapa kiasi kikubwa cha fedha.

Chanzo hicho kilidai kuwa, lengo la vikao vinavyoshirikisha wajumbe hao ni kuhakikisha mgombea wao anaingia Ikulu kwa gharama yoyote na kupewa maelekezo ya kufanya.

Maelekezo hayo ni pamoja na kuhoji sababu za mgombea huyo kupewa adhabu kwa kosa la kuanza kampeni mapema, kuing'oa Kamati Kuu inayoongozwa na Rais Kikwete na Sekretarieti ya CCM inayoongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Abdulrahman Kinana kwa tuhuma za kutomshauri Mwenyekiti wa chama kuhusu umuhimu wa kuitisha vikao.

Rafiki wa mgombea huyo, anadaiwa kuwataka wajumbe hao kumuombea kura mgombea wao katika vikao vya chama kwa
maelezo kuwa, yeye ndiye mwenye kuimudu nafasi hiyo kuliko wagombea wengine katika mchakato huo.

Baadhi ya wajumbe hao, wanadaiwa kupewa kazi ya kuwachafua na kuwadhalilisha viongozi wa CCM ngazi ya juu akiwemo Rais Kikwete, Bw. Philip Mangula (Makamu mwenyekiti wa CCM-Bara), Bw. Kinana na Bw. Nape Nnauye (Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Taifa).

Inadaiwa kuwa, zaidi ya sh. bilioni 10.7 zimepangwa kutumika ili kuwahonga wajumbe 370 wa NEC, wajumbe 2,011 wa Mkutano Mkuu pamoja na wajumbe 270 wa Zanzibar ili kuhakikisha chama kinamteua mgombea huyo kuwania urais Oktoba mwaka huu.

Taarifa zaidi zinadai kuwa, lengo la kutaka kuwafukuza wajumbe wote wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya chama ni kutoa fursa ya kuchagua wajumbe wapya ambao watasimamia mchakato wa kupitisha jina la mgombea wao kwa tiketi ya CCM.


  Chanzo Gazeti la Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa