Home » » MGODI WAAGIZWA KUNUNUA MASHINE KUKAGUA WATUMISHI.

MGODI WAAGIZWA KUNUNUA MASHINE KUKAGUA WATUMISHI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMPUNI ya wazawa ya Sky Associate iliyonunua mgodi wa TanzaniteOne ulioko Mirerani wilayani hapa, imeagizwa kununua mashine za kisasa za ukaguzi kwa ajili ya kukagua wafanyakazi wake wanapoingia na kutoka mgodini badala ya sasa kukaguliwa kwa kuvua nguo.
Aidha, Menejimenti ya kampuni hiyo imekiri kucheleweshwa kwa fedha katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Hayo yalibainika juzi katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Mirerani mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mikoa mitatu ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla.
Makala alifikia uamuzi huo baada ya wafanyakazi kutangaza mgomo wao ulikuwa uanze jana huku wakitoa madai 14 yakiwamo ya upigaji nguzo usio salama kwenye migodi, kutopelekewa makato yao ya bima ya afya na NSSF kwa wakati kwani wanadaiwa zaidi ya Sh milioni 300 katika hifadhi ya jamii.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini (Tamico), Hagai Daniel alidai wananyanyasika ikiwemo kuvuliwa nguo kwa madai ya kudhibiti wizi wa madini.
Pia alisema makato yao ya bima ya afya pamoja na NSSF hayaendi kwa wakati na pale wanapoumwa wafanyakazi wanashindwa kutibiwa kutokana na ukosefu wa fedha, hivyo kutokana na ukosefu huo wa malipo ya matibabu kwa wakati, umesababisha kukosa huduma za matibabu kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa.
“Hatukubali kwa nini kampuni ichukue mgodi na kukubali kulipa madeni yaliyoachwa na mwekezaji na kwa nini watudhalilishe kwa kutuvua nguo, pia kampuni kuwa na mikataba miwili tofauti ya kufanya kazi,” alidai Daniel.
Baada ya madai hayo kuwasilishwa na wafanyakazi hao, Makala alisisitiza kampuni hiyo kuwa na mawasiliano na wafanyakazi hao ikiwemo kununua mashine za ukaguzi zisizo na madhara, lakini pia alitoa miezi mitatu kuhakikisha fedha za hifadhi ya jamii zinalipwa kwa wakati ili kila mfanyakazi afanye kazi kwa ufanisi.
Naye Meneja Rasilimali Watu, Laizer Isiri alikiri kutopeleka fedha hizo kwa wakati na kusisitiza watahakikisha zinapelekwa, na kuongeza kuwa yapo madai ya wafanyakazi ya mishahara na malimbikizo ya NSSF tangu mwaka 2014 ambayo hayajalipwa ikiwa ni deni lililorithiwa kutoka TanzaniteOne kabla ya kununua hisa zake.
 CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa