Home » » RC MNYETI AKAGUA UJENZI UKUTA UNAOZUNGUKA MIGODI YA MADINI YA TANZANITE MIRERANI.

RC MNYETI AKAGUA UJENZI UKUTA UNAOZUNGUKA MIGODI YA MADINI YA TANZANITE MIRERANI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, ameanza rasmi kazi Mkoani humo kwa kukagua ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli. 

Mnyeti alitembelea eneo hilo na mwenyeji wake mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo. Alipongeza kasi ya maandalizi ya ujenzi huo kwani kila sehemu aliyokagua ambapo ukuta utapita aliwakuta vijana hao wa JKT wana ari na hamasa ya utendaji kazi. 
"Kwa namna vijana wetu wanajeshi wanavyoonekana kwenye maeneo yote niliyopitia wanaonyesha wataimaliza kazi hii ndani ya muda mfupi tofauti na agizo la miezi sita lililotolewa na Rais Magufuli," alisema Mnyeti.Aliwaahidi kutoa ushirikiano kwa jambo lolote lile watakalokuwa wanalitaka kwenye serikali ili kuhakikisha agizo hilo la Rais Magufuli linatekelezeka kwa wakati husika. 
Kamanda wa operesheni ukuta Mirerani, Kanali Festus Mang'wela alimhakikishia mkuu huyo wa mkoa kuwa vijana wote wanaojenga ukuta huo watafikishiwa ujumbe huo wenye lengo la manufaa ya kulinda afya zao. Kanali Mang'wela alisema ukuta huo wenye kilometa 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu unatarajiwa kuanza kujengwa rasmi Novemba 6 mwaka huu. 

Alisema wanatarajia mkuu wa JKT Meja jenerali Michael Isamuhyo ndiye atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa ukuta wanaotarajia kuujenga kwa muda usiopungua miezi sita. Alitoa shukrani kwa serikali ya wilaya ya Simanjiro kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa askari hao wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo la maandalizi ya ujenzi wa ukuta huo. 
Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary akisoma taarifa ya Wilaya hiyo kwa mkuu wa mkoa huo alisema wanashirikiana ipasavyo katika maandalizi ya ujenzi wa ukuta huo. Alisema serikali ya wilaya ya Simanjiro na uongozi wa JWTZ wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika ipasavyo na kwa wakati muafaka. 

Alisema ukuta huo utachangia kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo ambayo huuzwa yakiwa ghafi au kusanifiwa na kuuzwa na madalali na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi. Alisema katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, wamefanikisha uanzishwaji wa ujenzi wa ukuta na kupatikana eneo la mnada wa madini ya Tanzanite Mirerani. 
"Hadi hivi sasa imeshafanyika minada minne ya madini ya Tanzanite jijini Arusha na serikali kuu na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro zikapata kodi ya mapato na kodi ya huduma ila minada ijayo itafanyika Mirerani," alisema Omary. 
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (wa pili kushoto) akitembelea kambi ya wanajeshi wanaojenga ukuta wa kuzunguka madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro (kushoto) ni Mkuu wa wilaya hiyo Zephania Chaula na (wapili kulia)  ni msimamizi wa ujenzi huo kanali Festus Mang'wela kwenye ziara yake ya kwanza Mkoani humo.  
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kushoto) akimsikiliza msimamizi wa ujenzi wa ukuta unaojengwa kuzunguka madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Kanali Festus Mang'wela, (katikati) baada ya kutembelea zahanati ya kijiji cha Naisinyai ambapo madaktari wa JWTZ wanatoa huduma za afya. 
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kulia) akikagua maandalizi ya ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro. 
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kushoto) akikagua maandalizi ya ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro. 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kushoto) akikagua ramani ya ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa