Ahmed Makongo, Serengeti
DIWANI wa Natta ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Jumanne Kwiro, amesema anakusudia kupeleka hoja binafsi katika kikao kijacho cha baraza la madiwani, ili kuvunjwa mkataba kati ya halmashauri hiyo na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Grumeti Reserve kwa kushindwa kutimiza masharti ya mkataba huo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Kwiro alisema mkataba huo uliofungwa mwaka 2007 kati ya Kijiji cha Makundusi, na Kampuni ya Grumeti Reserves, unabainisha kampuni hiyo, imeshindwa kutekeleza mambo mengine yaliyoko kwenye mkataba huo.
Aliwaomba wananchi pamoja na madiwani kumuunga mkono, ili kuhakikisha mkataba huo unavunjwa.
“Kikao kijacho lazima niwasilishe hoja binafsi ili kuomba mkataba huo uvunjwe kwani tunaona Grumeti imeshindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba,” alisema.
Alisema mkataba huo unasema faida yote ambayo kampuni hiyo inapata watairudisha kwa jamii kwa shughuli za maendeleo, lakini kinyume chake kampuni hiyo haifanyi hivyo na kila mara imekuwa ikipiga chenga ikiwa ni pamoja na kutolipa kijiji sh milioni 200 za uwindaji wa kienyeji kwa wakati.
Alisema mkataba huo unasema fedha hizo (sh milioni 200) zilipwe kila mwaka, lakini kampuni hiyo imekuwa ikilizilipa kwa kujisikia, ambapo hadi sasa za mwaka huu bado hazijalipwa.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, John Ng’oina, alisema kuwa jambo hilo linazungumzika kupitia kwenye vikao vya halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kuzungumza na kampuni hiyo, ili kutekeleza yaliyomo kwenye mkataba huo.
Meneja Mahusianao katika kampuni hiyo, Richard Andasikoi, pamoja na kukataa kuwa si msemaji wa kampuni, alikanusha madai kwamba kampuni hiyo haitekelezi mambo yaliyomo kwenye mkataba huo na kwamba ushahidi wa kutosha upo, kwa sababu mara kwa mara wamekuwa wakichangia shughuli za maendeleo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment