Home » » Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari; JK Aishukuru Kampuni Ya Simu Ya Vodacom Kwakuchangia Mradi Wa Kuhifadhi Mbwa Mwitu

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari; JK Aishukuru Kampuni Ya Simu Ya Vodacom Kwakuchangia Mradi Wa Kuhifadhi Mbwa Mwitu


Mhudumu wa Mbwa mwitu hao akiandaa chakula cha mwisho kwa ajili ya Mbwa mwitu kumi na Moja, kabla hawajarudishwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012 baada ya kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi huo, katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara
Mbwa mwitu kumi na Moja wakipata mlo wao wa mwisho kabla ya kurudishwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012  baada ya kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project,  katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
                                   TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kwa kuchangia katika mradi wa kuhifadhi mbwa mwitu katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mradi unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project, kwa dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.



Rais ametoa shukrani hizo Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom hapa nchini Bw. Rene Meza, Ikulu Dar-Es-Salaam, walipokutana jana jioni, Ijumaa Agosti 31,2012




"Napenda kutoa shukrani zangu kwa Vodacom kwa msaada huu mkubwa, tunashukuru kwa jitihada zenu kubwa katika hili" Rais amesema.




Naye Mtendaji Mkuu wa Vodacom amemhakikishia Rais kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo, elimu na Afya.




“Tunajisikia faraja sana kuwa miongoni mwa washirika wa mradi huu. Ni heshima kwetu na tuko makini nao, tunataka kuendelea na mradi huu" Bw, Rene Meza amemhakikishia Rais.





Tayari mbwa mwitu kumi na Moja, wamerudishwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012 baada ya kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi huo, katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.




Wadau wengine walioshiriki na kufanikisha zoezi hilo ni pamoja na Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Frankfurt Zoological Society , Grumeti Fund na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.




Kuachiwa kwa Mbwa Mwitu hao 11 walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya wanyama hao katika mbuga hiyo maarufu duniani. Hivi sasa kuna makundi 11 yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya Ngorongoro, yakifanya jumla ya Mbwa Mwitu 200.




Mtafiti wa Magonjwa ya Wanyama kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyama (TAWIRI) Dkt. Ernest Mjingo, alimwambia Rais Kikwete kwamba katika Hifadhi ya Serengeti makundi ya Mbwa Mwitu yalikuwa yakionekana kwa wingi, lakini sasa yametoweka na mara ya mwisho Mbwa Mwitu wawili walionekana mwaka 1998.




Mtafiti huyo alisema Mbwa Mwitu wamekuwa wakitoweka kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao na kuugua magonjwa mbalimbali kama kichaa cha mbwa.




Dkt. Mjingo alisema baada ya kuachiwa Mbwa Mwitu hao, waliovishwa collar maalumu zenye redio, juhudi zitaendelea ili kupata makundi sita yenye Mbwa Mwitu takriban kumi kila moja, ikiwa ni hatua endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha uwepo wa wanyama hao mbugani humo.




Mbwa Mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa katika Bara la Afrika kuna Mbwa Mwitu wanaofikia 8,000 na Tanzania pekee inakadiriwa kuwa wanyama hao 3,500 katika mbuga mbalimbali nchini. Katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti walitoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.




Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
1 Septemba, 2012

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa