Home » » MGOGORO WA ARDHI KITETO WAUA WATU 5

MGOGORO WA ARDHI KITETO WAUA WATU 5

Mgogoro wa ardhi baina ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto, mkoani Manyara umesababisha vifo vya watu 15 na wengine 14 kujeruhiwa.
Idadi hiyo iliongezeka jana kufuatia watu sita kuuawa na mmoja kujeruhiwa wakati wa mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, wakulima wa Kiteto walisema kuwa mapigano hayo yalitokea jana katika vitongoji viwili ambavyo ni Laitimi na Lemenya ambavyo vipo katika hifadhi ya mbuga ya Embroi Murtangosi.

Walisema kuwa wafugaji jamii ya Kimasai walivamia vitongoji hivyo na kuanza kuchoma vibanda vya wakulima na kuwapiga kwa kutumia silaha na kuwaua.

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Machite, alisema kuwa jana asubuhi alipatiwa taarifa na vijana wake ambao walikuwa
shambani wakisema kuwa wamevamiwa na wafugaji hao na kuchoma nyumba zao na kwamba baadhi wamefariki.

Alisema kuwa mapigano hayo sasa yameingia katika sura ya tofauti kwani kuna kundi kubwa la jamii ya wafugaji wa Kimasai wakiwa na silaha za kivita ndio waliofanya tukio hilo.

Alisema kuwa yeye analima katika eneo la Laitimi ambalo wakulima wanalima ndipo jamii ya wafugaji wa Kimasai walipowavamia na wanafanya matukio hao wakijua kabisa wote wanatakiwa kuondoka.

Kwa upande wake, Abdi Mussa, alisema kuwa mapigano hayo yalitokea katika vitongoji hivyo na taarifa aliyoipata ni kuwa watu 11 wamekufa kwa kushambuliwa na wafugaji hao.

”Mimi kinachonishangaza hawa wafugaji inakuwaje wafanye kitendo hiki wakati juzi tu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo, alitoa tamko la kututaka wote tutoke katika hifadhi,” alisema.

”Eti wewe ni mwizi itakuwaje unamuadhibu mwizi mwenzako...Hawa wanapewa kichwa na nani au kwakuwa wametoa mamilioni ya fedha kwa viongozi ndio maana wanafanya hivi, wanaona wanahaki,” alisema mkulima huyo.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Kamanda wa polisi mkoani Manyara, Akilimali Mpwapwa, alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo katika hifadhi ya Embroi Murtangosi na kueleza kuwa bado hajapata idadi kamili ya watu waliokufa. Kamanda Mpwapwa alisema kuwa amepata taarifa tofauti tofauti za vifo, hivyo bado hajapata taarifa kamili na tayari amemtuma OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) kwenda katika eneo la tukio.

Kamanda Mpwapwa alisema kuwa atatoa taarifa mara baada ya OCD kurejea kutoka katika eneo la tukio.

Aliwataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kuishi katika hali ya utulivu katika kipindi hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Matha Umbulla, alithibitisha kutokea mapigano katika eneo hilo jana asubuhi na kwamba taarifa alizozipata awali zinasema watu sita wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa.

Alisema maiti na majeruhi walifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.
“Hapa nipo njiani naelekea eneo la tukio maana ni mbali kutoka hapa wilayani, lakini kwa taarifa niliyopewa na OCD, maiti sita na majeruhi mmoja wamefikishwa hospitali,” alisema na kuongeza:

“Ninashangazwa na inaniumiza akili ni kitendo hiki na sijui ni kwa nini wananchi wanakuwa wakaidi kusikia kauli za viongozi.” Desemba 16, mwaka huu watu watano waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa. Januari 3, mwaka huu, mapigano yalizuka tena na watu wanne waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa.

 Mgogoro huo umedumu miaka nane huku jitihada mbalimbali za kuusuluhisha zikishindwa kuzaa matunda.  
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa