MBUNGE wa Viti Maalumu, Moza Abeid (CUF), ameishambulia serikali na
kueleza kuwa migogoro mingi ya ardhi ambayo inaonekana kupamba moto
nchini inachangiwa kwa kiasi kikubwa na serikali.
Moza alisema kuwa serikali inahusika kutokana na kushindwa kuweka
kipaumbele katika upimaji wa ardhi, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na
mipango ya kutoa fidia kwa watu ambao wanatakiwa kuhamishwa kutoka
katika maeneo yao.
Mbunge huyo alitoa kauli wakati wa kujadili jinsi ya kutatua migogoro
ya mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Pori la Akiba la
Mkungunero na vijiji vya jirani.
Akichangia Moza alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa baadhi ya watu
kudai kuwa migogoro hiyo inasababishwa na wanasiasa lakini tuhuma hizo
si sahihi, kwa kuwa chanzo kikubwa ni serikali.
Moza alilazimika kueleza hayo baada ya Mbunge wa Kondoa Kaskazini,
Zabein Mhita (CCM), kueleza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao
wanachochea kuwepo kwa mgogoro wa mipaka hususan katika maeneo ya
hifadhi.
Zabein alisema wapo wanasiasa ambao wanakwenda kwa wananchi ambao
wapo katika maeneo hayo na kuwachochea kuendelea kufanya shughuli zao
za kibinadamu, hatua inayochangia kuwepo kwa machafuko pale
wanapoondolewa.
Kauli hiyo ilipingwa vikali na baadhi ya washiriki wa mkutano huo
ambapo Moza alidai kuwa madai ya mbunge huyo hayana msingi anayetakiwa
kulaumiwa ni serikali kwa kushindwa kutoa kipaumbele kwa ajili ya
kupima mipaka.
Mbali na hilo alisema kuwa serikali imekuwa ikijichanganya yenyewe
kwa kushindwa kupima mipaka na wakati mwingine kutoa hati ya matumizi
ya ardhi kwa wananchi na wakati huo kutoka hati ya kutangaza kuwa ni
hifadhi.
Katika mkutano huo wataalamu wengi ambao waliwasilisha mada kuhusu
migogoro ya mipaka waliituhumu moja kwa moja serikali kwa kushindwa
kutenga fedha kwa ajili ya kupima mipaka.
Naye Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema njia
pekee ya serikali kuondokana na migogoro ni kutumia busara ya kutenga
maeneo ambayo yatawapa fursa wakulima kulima, wafugaji kufuga pamoja na
kuweka mipaka sahihi ya hifadhi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment