Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KILA mtu anazungumzia au kama hazungumzii yumkini ameshasikia
watu au vyombo vya habari vikizungumzia juu ya kompyuta, teknohama au
tehama au simuakili, ipod, amazon kindle, na mambo kama hayo. Ila sina
uhakika kama wengi wetu tunafahamu ukubwa wa mapinduzi na mabadiiko
ambayo yanaashiriwa na uwepo na ujio wa vifaa na zana hizi.
Kwa takwimu zilizopo hivi leo ilhali kampuni ya
Simu Tanzania (Tanzania Telecommunication Company Ltd au TTCL ikiwa na
simu zake za ofisini na za nyumbani. Simu za kiganjani au simupopote
zilianza watu 227,424, walipoingia sokoni kuanzia miaka ya kati ya 1990
sasa wameipaisha idadi ya wamiliki wa simu kufikia zaidi ya milioni 28
na bado inaendelea kukua. Kwa hiyo badiliko kuu la kwanza ambalo liko
wazi kwa kila mtu kuona na kusikia ni kwamba zaidi ya nusu ya Watanzania
hivi leo wana mawasiiano ya simu kupitia mtandao huu au ule.
Kinachoendelea hivi sasa ni kwa Watanzania wengi
kuanza kugura toka kwenye simu za mkononi zisizokuwa na akili kwenda
kwenye simu za mkononi zenye akili. Simu ambazo kwa kiasi kikubwa
zinaweza kutumika kama vile ni kompyuta ndogo mkononi mwa mtu
anayeitumia.
Tangu mwanzo wakati kompyuta zinaingia nchini
kulikuwa na wazee waliokuwa wakihofia hata kuzigusa achilia mbali
kuzitumia. Jiulize, sasa zinakuja simu za mkononi ambazo zimefanana na
kompyuta kwa kiasi kikubwa je, pengo kati ya wanaoona rahisi kuzitumia
na wanaoziogopa limekua kiasi gani.
Ninaamini hivi sasa kuna walakini na udhaifu
mbalimbali unaotokana na wanaoshika nafasi za uongozi katika serikali,
vyama vya siasa, vyuo vikuu na shule, mashirika ya umma na mashirika
binafsi kuwa ngumbaru katika matumizi ya teknolojia au teknohama wakati
watumishi wa chini ambao wengi wao ni vijana ni stadi wa kutumia
kompyuta na simu za mkononi za kisasa.
Kompyuta, simuakili, intaneti na vikorokoro vyake
vimezua changamoto mpya katika uendeshaji shughuli za uchumi, jamii,
siasa na utamaduni na hata teknolojia yenyewe.
Mtawala au meneja mzuri hivi leo penda usipende
lazima pamoja na uweledi na ujuzi wake wa menejimenti awe pia anajua
kutumia kompyuta na teknohama kwa mapana na marefu. Teknolojia ya
taipuraita ingawa bado iko katika baadhi ya maofisi ya serikali ni
teknolojia inayoelekea kwenda kutupa kwenye jalala la takataka baada ya
muda siyo mrefu.
Changamoto kubwa na ambayo mimi ninaihofia ni ile
itakayoletwa na tofauti ya kasi katika utendaji kazi baina ya vijana na
wazee. Vijana watakaokuwa wanataka mambo yao yaende haraka haraka zaidi
na wazee ambao kwa hofu yao ya teknohama na teknolojia nyingine zilizopo
watataka muda mrefu zaidi katika kuamua na kutekeleza uamuzi
uliokwishafanyika.
Kwa upande mwingine wazee watakuwa wakienda
kigoigoi na wataendelea kukumbatia ukiritimba, vyeo, ukubwa na ufahari
ilhali vijana watapigania kuwepo uwazi, ushindani, uchangiaji na
ushirikiano katika nyanja zote za kazi ili kupafanya mahala pa kazi kuwa
sehemu inayowatendea haki wananchi wengine wasiopo hapo katika jamii
husika. Wazee watang’ang’ania ukirimba na kuwa na woga wa kugawa pato la
taifa ili kuleta uwiano katika jamii kwa kasi zaidi kwa kuwa tamaa ya
mali, ulimbikizaji na kutokuachia fursa tayari kumeshawalemaza.
Jambo hili litatokea katika kupanga, kutekeleza,
kufuatilia na kudhibiti shughuli zinazofanyika katika eneo husika.
Mabadiliko haya yanaweza kuzusha mihemuko na misongo baina ya wazee na
vijana kutokana na misuguano ya kimawazo, kiuamuzi, kimawasiiano na
kiteknolojia.
Kwa sababu hii upo uwezekano mkubwa kwa viongozi
kutaka kupunguza kasi ya kuenea na kukua kwa matumizi ya teknolojia mpya
kutokana na hofu za kiuongozi na kisiasa na siyo za kiuchumi na
kimaendeleo jamii.
Hata hivyo, kitendo cha kuzuia kasi ya kukua na
kuenea kwa teknolojia ni kitendo kinachofananishwa na mtu kupambana na
ukuta kwani mabadiiko hayazuiliki. Na ni dhahiri katika dunia ya
ushindani wale watakaoshindwa kuchangamkia matumizi ya teknoljia fulani
watajikuta siku zote wako nyuma ya wale wanaokubali na kuitumia
teknolojia mpya haraka zaidi.
Katika kipindi cha mpito inawezekana kuwa na watumishi au
rasilimali watu ambayo ni mbumbumbu wa teknohama, lakini katika miezi
michache ijayo na wala siyo miaka, watumishi wasiojua teknohama watakuwa
ni mzigo kwa wizara, idara, mashirika na taasisi walizomo. Kwa maneno
mengine, fumba na kufumbua mtu ambaye atakuwa ngumbaru wa teknoljia
muhimu zinazotumika katika shughuli zinazomhusu atakuwa ni sawa na yule
mnyama aliyepitwa na wakati na kuzikwa kwenye kaburi la sahahu la
teknoljia duniani.
Hii ina maana hakuna tena nafasi kwa wazee kukwepa
matumizi ya teknohama na wakiwazuia au kuwakwaza vijana watajikuta
wanajikwamisha wenyewe na maendeleo ya taasisi wanazoziongoza.
Ili kuleta kasi katika matumizi ya teknohama
ningeliishauri serikali iingie ubia na makamapuni ya ndani na nje ya
nchi ili kuwa na madarasa maalumu ya ngumbaru wa teknohama ili tuondoe
tofauti kati ya watumishi wanaojua teknohama na wale wasiojua ili
kuwatendea Watanzania haki kutokana na yale yanayowezekana kufanyika
endapo mtu atakuwa ana weledi na ujuzi wa teknohama katika kazi zake
tofauti na yule asiyejua kitu.
Pepe: sammymakilla@hotmail.coom
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment