Hali ya joto nchini imeongezeka kutoka nyuzi 0.2 mwaka 1990 hadi kufikia nyuzi joto 0.6 kwa mwaka huu, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, huku wastani wa joto kwa dunia ukiwa ni nyuzi joto 0.85.
Kadhalika, wastani wa kina cha bahari kimeongezeka kwa urefu wa sentimeta 19 kwa miaka 30 iliyopita.
Imeelezwa kuwa hali hiyo imesababishwa na ongezeko la viwanda duniani pamoja na kuongezeka kwa gesi ya ukaa kunakotokana na ukataji wa miti.
Hayo yameelezwa na wataalamu wa mabadiliko ya tabia nchi waliokutana jijini Dar es Salaam katika kongamano lenye mada ‘ukuaji wa uchumi unaohimili mabadiliko ya tabia nchi’.
Mtaalamu mshauri kutoka Afrika ya kati, Dk. Yoruba Sokono, alisema Tanzania kwa sasa joto limeongezeka kwa kasi na kueleza kuwa kuna uwezekano hata wa kufika nyuzi joto tatu ifikapo mwakani ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Philipe Dongier, alisema katika kongamano hilo wataalamu hao watajadiliana na kupendekeza hatua thabiti za kuchukua pamoja na kuandaa sera, mipango na uwekezaji nchini Tanzania.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binlith Mahenge, alisema serikali imejipanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment