Home » » WALIMU WAPYA KARIBUNI TUPATE WATAALAMU WENGI

WALIMU WAPYA KARIBUNI TUPATE WATAALAMU WENGI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MIONGONI mwa habari njema zilizoripotiwa na vyombo vya habari jana ni tangazo la serikali la kuanza kwa ajira mpya za walimu, zinazotarajiwa kuanza Mei Mosi mwaka huu.

Hata hivyo katika tangazo lake, serikali imeweka wazi kwamba walimu hao wapya, watakaopata ajira katika siku hiyo muhimu kwa wafanyakazi yaani Mei Mosi, wasitarajie kupangiwa katika maeneo ya majiji, manispaa na miji.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira mwezi ujao ni 31,056 ambapo walimu wa ngazi ya cheti ni 11,795, stashahada 6,596 na wenye shahada 12,665.
Serikali ikitangaza ajira hizo imesema kwa mwaka huu zimechelewa kutoka kutokana na Tamisemi na Wizara ya Elimu na Mafunzo, kufanya ufuatiliaji wa kina hadi katika ngazi za shule ya msingi ili kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu kwa kila halmashauri na shule.
Mbali ya hilo serikali imesisitiza kuwa walimu wapya wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya Majiji, Manispaa na Miji, kutokana na idadi ya walimu waliopo kuwa kubwa na inakidhi mahitaji huku maeneo yaliyopewa kipaumbele ni vijijini na halmashauri, ambazo zina mahitaji na upungufu mkubwa wa walimu.
Kwetu sisi tunaziita habari hizi kuwa ni njema kutokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ikiwa ni hatua hiyo kulenga kuongeza idadi ya walimu katika mfumo wa ufundishaji, hatua ambayo kwa kiwango fulani itasaidia kupunguza uchache wa walimu katika shule mbalimbali.
Hakuna shaka kwamba walimu hawa watakapoanza kazi na kwa vile tayari serikali imesema watapangiwa katika shule za vijijini na katika halmashauri wilayani, ni wazi kuwa ongezeko lao litasaidia kuongeza idadi ya walimu katika maeneo hayo, ambayo yanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za uhaba wa wataalamu.
Sisi kama chombo kinachojihusisha na mawasiliano katika jamii, tunazielewa fika changamoto za uhaba wa walimu katika maeneo ya vjijini, na mara kadhaa tumekuwa tukiibua taarifa zinazohusu shule zenye matatizo makubwa ya walimu, zana za kufundishia na zana za kujifunzia.
Kwa vile Tamisemi imesema kuwa kuchelewa kutangazwa kwa ajira hizo, kunatokana na ufuatiliaji wa kina uliofanywa ili kubaini kwa uhakika mahitaji halisi ya walimu kwa kila halmashauri na shule, ni imani yetu kuwa walimu husika watapangiwa katika maeneo muafaka.
Tunataraji sasa zile shule zilizokuwa zikiripotiwa kuwa na Mwalimu Mkuu peke yake, anayefundisha kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba, zitafikiwa na sasa tutasikia habari mpya za shule hizo kupunguziwa mzigo uliokuwa ukiwakabili.
Pamoja na pongezi hizo, tunatoa rai kwa serikali kuendelea kuitupia macho sekta ya ualimu ili kutoa ajira nyingi zaidi kwa walimu kila mwaka kwa lengo la kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa walimu katika shule za msingi, linafutika kabisa na kubakia kuwa historia.
Ni kweli kwamba Taifa linahitaji madaktari wengi, wahandisi mitambo wengi, marubani wengi, wanasayansi wengi, wahasibu wengi, lakini ili hao waweze kupatikana ni lazima wawepo walimu wengi, ambao watakuwa chimbuko la kuwapata wataalamu hao wengi zaidi.
Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa