Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMPUNI ya wazawa ya Sky Associate iliyonunua mgodi wa TanzaniteOne
ulioko Mirerani wilayani hapa, imeagizwa kununua mashine za kisasa za
ukaguzi kwa ajili ya kukagua wafanyakazi wake wanapoingia na kutoka
mgodini badala ya sasa kukaguliwa kwa kuvua nguo.
Aidha, Menejimenti ya kampuni hiyo imekiri kucheleweshwa kwa fedha
katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Mfuko wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF).
Hayo yalibainika juzi katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Mirerani
mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mikoa mitatu ya Manyara,
Kilimanjaro na Arusha iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos
Makalla.
Makala alifikia uamuzi huo baada ya wafanyakazi kutangaza mgomo wao
ulikuwa uanze jana huku wakitoa madai 14 yakiwamo ya upigaji nguzo usio
salama kwenye migodi, kutopelekewa makato yao ya bima ya afya na NSSF
kwa wakati kwani wanadaiwa zaidi ya Sh milioni 300 katika hifadhi ya
jamii.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi
wa Migodini (Tamico), Hagai Daniel alidai wananyanyasika ikiwemo
kuvuliwa nguo kwa madai ya kudhibiti wizi wa madini.
Pia alisema makato yao ya bima ya afya pamoja na NSSF hayaendi kwa
wakati na pale wanapoumwa wafanyakazi wanashindwa kutibiwa kutokana na
ukosefu wa fedha, hivyo kutokana na ukosefu huo wa malipo ya matibabu
kwa wakati, umesababisha kukosa huduma za matibabu kuanzia mwaka 2015
mpaka sasa.
“Hatukubali kwa nini kampuni ichukue mgodi na kukubali kulipa madeni
yaliyoachwa na mwekezaji na kwa nini watudhalilishe kwa kutuvua nguo,
pia kampuni kuwa na mikataba miwili tofauti ya kufanya kazi,” alidai
Daniel.
Baada ya madai hayo kuwasilishwa na wafanyakazi hao, Makala
alisisitiza kampuni hiyo kuwa na mawasiliano na wafanyakazi hao ikiwemo
kununua mashine za ukaguzi zisizo na madhara, lakini pia alitoa miezi
mitatu kuhakikisha fedha za hifadhi ya jamii zinalipwa kwa wakati ili
kila mfanyakazi afanye kazi kwa ufanisi.
Naye Meneja Rasilimali Watu, Laizer Isiri alikiri kutopeleka fedha
hizo kwa wakati na kusisitiza watahakikisha zinapelekwa, na kuongeza
kuwa yapo madai ya wafanyakazi ya mishahara na malimbikizo ya NSSF tangu
mwaka 2014 ambayo hayajalipwa ikiwa ni deni lililorithiwa kutoka
TanzaniteOne kabla ya kununua hisa zake.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment