Home » » Utandazaji bomba la gesi Mtwara-Dar wakamilika kwa asilimia 39

Utandazaji bomba la gesi Mtwara-Dar wakamilika kwa asilimia 39

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
 
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema ujenzi wa kutandaza na kuunganisha mabomba ya gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Kinyerezi, jijini Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 39 sawa na umbali wa kilomita 200 hadi Desemba mwaka jana.

Kasi ya ujenzi inapungua kutokana malighafi kuchelewa kufika katika eneo la ujenzi, hususani namna ya upatikana wa vibali vya kusafirisha vifaa vya ujenzi wa bomba kwa wakati kutoka kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad).


Meneja mradi wa ujenzi wa bomba hilo kutoka TPDC, Kapuulya Musomba, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana.


Alisema ujenzi wa mbomba hilo unaendelea vizuri na kuomba ushirikiano na Tanroads ili vibali vinavyotolewa kwa siku 14,vipatikane kwa wakati ili kuharakisha ujenzi wa mradi huo mkubwa ambao unasubiriwa nchini.


“Desemba 19,mwaka jana, asilimia 80 ya mabomba yaliwasili nchini kutoka nje ya nchi, yatafanikisha kutandazwa kwa kilomita 440 kati ya kilomita 547, hivyo kiasi cha bomba kilichobaki kitawasili hivi karibuni,” alisema.


Musomba alisema mradi wa kutandaza mabomba ya gesi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kwamba baada ya ujenzi, mitambo mbalimbali itafanyiwa majaribio kabla ya kuanza matumizi ya uzalishaji wa nishati hiyo.


Aidha alisema kazi iliyopo ni kupambana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kuchelewa kwa mabomba bandarini kwa ajili ya kusubiri nafasi bandari kavu kutokana na msongamano wa mizigo. 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa