Home » » TRA yafundwa wafanyabiashara

TRA yafundwa wafanyabiashara

Babati. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Manyara, imewataka wafanyabiashara kuendelea kutumia mashine za kielektroniki (EFD) ili kuwarahisishia utunzaji kumbukumbu na ukadiriaji kodi.
Akizungumza kwenye jukwaa la wadau juzi, Ofisa Kodi Msaidizi wa TRA mkoani Manyara, Fredy Peter alisema mashine hizo zina uwezo wa kutunza kumbukumbu za mauzo, ununuzi na mali za biashara bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano na kuondoa usumbufu wa kuchapisha vitabu vya risiti.
“Sheria inamtaka mfanyabiashara anyeuza au kutoa huduma ya sh5000 na zaidi atoe risisti na pia atalazimika kuchapisha vitabu vya risiti mara zote na sasa zinatumika mashine ili kuondokana na uchapishaji wa vitabu,” alisema.
Alisema mfumo huo ni wa awamu ya pili kutekelezwa na unawalenga wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye uongezeko la thamani (VAT) ambao mauzo ghafi yao kwa mwaka ni sh14 milioni na zaidi.
Aliwataja walengwa wa awamu hiyo kuwa ni wenye maduka ya jumla, ya vipuri, mawakili, wafanyabiashara wa mbao na migahawa mikubwa, maduka ya simu, baa na vinjwaji baridi, studio za picha, wauzaji wa pikipiki na maduka makubwa ya nguo.
Nao, wadau hao waliutaka uongozi wa TRA kufuatilia makampuni matatu ya usambazaji wa mashine hizo ambayo ni Maxocom Africa, Webtechnologies na Power Computers ili kuhakikisha wanazitoa kwa muda muafaka.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa