HALMASHAURI ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara inakabiliwa na
changamoto ya utekelezaji wa ukusanyaji wa mapato ya zaidi ya sh bil.
31 kwa bajeti ya mwaka 2013/2014 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato.
Akizungumza katika mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani, Mwenyekiti
wa halmashauri hiyo, Nicodemus Tarimo alisema kuwa walikisia kukusanya
sh bil. 1.867 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani huku sh bil. 21.339
ikiwa ni mishahara ya watumishi na sh bil. 2.279 ni matumizi mengineyo
na miradi ya maendeleo ikiwa sh bil. 5.566.
Tarmo alisema kuwa hadi kufikia Novemba 2013 halmashauri hiyo
ilipokea zaidi ya sh bil. 10.292 sawa na asilimia 33 ya lengo la bajeti
hiyo, huku matumizi yote yakiwa ni zaidi ya sh bil. 10.034.
“Sh bil. 1.083 ni matumizi ya baki ya mwaka 2012/2013 na zaidi ya sh
bil. 8.95 ni matumizi ya bajeti ya mwaka 2013/2014 ambayo ni sawa na
asilimia 23 ya lengo,” alisema.
Alisema kuwa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji huo ni
pamoja na ruzuku kutoka serikali kuu kutokufika kwa wakati na wakati
mwingine kushindwa kufika kabisa hatua iliyokwamisha utekelezaji wa
miradi iliyokusudiwa.
Hata hivyo, alisema wameweka mikakati ya kukabiliana na changamoto
hizo na kwamba wataendelea kufuatilia na kuikumbusha serikali kuu
kuhusu umuhimu wa kutoa fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment