Manyara. Wakati Jeshi la Polisi likilazimika
kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya watu, Naibu Waziri wa Maendeleo
ya Mifugo na Uvuvi, Benedict Ole Nangoro, ametuhumiwa kuchochea mgogoro
wa wakulima na wafugaji Wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Aidha, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kiteto, Foca
Dinya, alituhumiwa kwa kuwapendelea wafugaji na kuwakandamiza wakulima
pindi inapotokea vurugu kati ya wakulima na wafugaji.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni katika mkutano wa
hadhara ulioitishwa na wakulima na wafugaji wa Kijiji cha Kibaya
wilayani humo.
Dalili za vurugu katika mkutano huo, zilianza
kuonekana baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Lusioki kuanza
kuhutubia ambapo wafugaji walisikika wakitaka kuuliza maswali.
Hata hivyo, Lusioki alilazimika kuwatuliza kwa
kuwaeleza mkutano huo unalenga kuzungumzia matatizo yanayowakabili,
hivyo wangepewa nafasi ya kuuliza maswali baada ya yeye kuhutubia.
Licha ya ahadi hiyo, upande wa wafugaji uliendelea
kudai huku baadhi yao wakiendelea kuwafukuza wakulima waliokuwa wamekaa
upande waliokuwa wamekaa.
“Mkutano huu ni wakulima na wafugaji, hamna haja ya kubaguana mnaweza kuchanganyika kwa pamoja,”alisikika akisema Lusioki.
Kauli hizo zilionekana kuzidi kuwachefua wafugaji,
hali ambayo ilimlazimu Dinya kuingilia kati kwa kuchukua kipaza sauti
na kutangaza mkutano huo umevunjika.
Hata hivyo, wakulima na wafugaji waliendelea
kukusanyika katika vikundi barabarani, hali iliyolilazimu jeshi hilo
kuwatangazia watawanyike lakini walikaidi na ndipo walipofyatua mabomu.
Akizungumza na waandishi baada ya mkutano huo
kuvunjika, Lusioki, alisema Serikali inaweza kuumaliza mgogoro huo wa
Hifadhi ya Emboloi Murtangosi, kwa kuviachia vijiji kupanga matumizi
bora ya ardhi kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba nne na tano.
Nangoro alikanusha kuhusika na uchochezi na kusema mgogoro huo unasababishwa na watu kutoka nje ya wilaya hiyo.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment