WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, amepiga
marufuku tabia ya wafugaji wilayani hapa kuingiza mifugo kwenye mashamba
ya wakulima nyakati za usiku, kwani jambo hilo linaweza kusababisha
mauaji tena wilayani humo.
Tizeba alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
katika kijiji cha Lupopong’i, Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara ambapo
pia alizindua lambo la maji lililojengwa katika kijiji cha Olyapasei.
Lambo hilo limejengwa na serikali na kugharimu zaidi ya Sh milioni
737 na linalenga kuhudumia zaidi ya mifugo 350,000 pamoja na matumizi ya
binadamu. Alisema zipo fununu watu wameanza kulisha mifugo usiku kwenye
mashamba ya wakulima.
“Suala hilo liachwe litasababisha kuuana tena, Kiteto imekuwa na
migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro midogo inayoanzishwa lazima
ikemewe,” alisema.
Aliwataka wakulima na wafugaji kupendana na kuepuka mambo
yanayohatarisha usalama wao na kuwa kitu kimoja kwa kila mtu kulinda
heshima na mali ya mtu mwingine.
“Iwapo kila mmoja ataheshimu mali ya mtu mwingine na kuangalia mipaka
ya ardhi aliyotengewa, hakuna migogoro wala mambo yatakayotokea tena,”
alisema.
Pia Waziri huyo aliwataka wazee wa kimila kukaa na kuzungumza kuweka hali ya utulivu katika maeneo yao.
Alimtaka mhandisi wa maji atafute mbinu ya kusafisha maji ili kuweza kutumika kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Kuhusu utunzaji wa mazingira aliwataka wakulima na wafugaji kuheshimu
vyanzo vya mtiririko wa maji ili waweze kuvuna maji ya kutosha.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Mary Mashingo,
alisema awali wilaya hiyo ilikuwa na malambo 41 lakini kutokana na
uharibifu mkubwa wa mazingira, yameharibika na kubaki malambo saba.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Lailumbe Mollel
alisema wafugaji wamekuwa wakihamahama kutokana na kutafuta malisho na
maji, hata kusababisha watoto wa wafugaji kukosa masomo.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment