Imeandikwa na Eric Anthony
WAKATI chupa tupu za plastiki za maji ya kunywa zikionekana kuwa adui
wa mazingira, huku kwa kiasi fulani zikitoa ajira kwa vijana wanaookota
na kuziuza kwa kampuni zinazoyeyusha bidhaa hizo, kundi la akinamama
nchini limeibuka na ubunifu wa kipekee.
Wanawake hao wanatumia chupa hizo kwa ujenzi wa nyumba imara na za
kisasa, badala ya matofali yanayotengenezwa kwa saruji au udongo na
kisha kuchomwa kama ilivyozoeleka katika maeneo mengi.
Mapinduzi hayo ya kiteknolojia nchini, yameanza kuonekana katika
kijiji cha Msitu wa Tembo, Simanjiro mkoani Manyara ambako kikundi cha
wanawake 60 kinachoitwa Sala na Kazi, kimejenga nyumba ya vyumba viwili
inayotumika kwa biashara ya duka la kikundi hicho.
Hayo yamethibitishwa na Mwenyekiti wa kikundi hicho, Belsira Samwel
aliyezungumza na gazeti hili hivi karibuni na kuthibitisha kuwa ni kweli
wamefanikiwa kujenga nyumba kwa kutumia chupa za plastiki, za maji na
za soda, zenye ujazo wa lita moja na nusu.
Alisema, mbali ya upatikaji kirahisi wa malighafi hiyo mpya katika
ujenzi, inasaidia pia utunzaji wa mazingira. Mathalani, anasema ili
kujenga nyumba hiyo ya vyumba viwili, walitumia chupa 4,500 tu, huku
ujenzi wote ukigharimu chini ya Sh 300,000 na kwamba gharama kubwa
ilikuwa katika kupaua, hasa kwa ununuzi wa mbao na mabati.
“Ni ujenzi wa kisasa, lakini nafuu na unaosaidia uhifadhi wa
mazingira,” anasema Mwenyekiti huyo ambaye baada ya kufanikisha ujenzi
wa nyumba ya vyumba viwili, aliongeza kuwa, wanakusudia kufyatua majengo
zaidi ya miradi, likiwemo la kuhifadhia baiskeli zaidi ya 66 za mradi
wa kikundi hicho ambacho huzikodisha kwa wanakijiji wengine.
ZINAVYOGEUZWA ‘TOFALI’
Mwenyekiti huyo alisema wakati wa ujenzi, chupa hizo hujazwa udongo
uliochekechwa na kufungwa vizuri, hivyo kutumika kwa ujenzi kwa kutumia
udongo na saruji kiasi ili kushikanisha chupa, kama inavyokuwa katika
ujenzi wa matofali.
Kwa mujibu wa wataalamu wa aina hiyo ya ujenzi, nyumba huwa imara,
zinaweza kuhimili mtikisiko wa ardhi, moto lakini pia wakati mwingine
hazipenyezi risasi kirahisi. Mbali ya kutumia chupa hizo katika ujenzi
wa nyumba, wabunifu katika nchi mbalimbali wamekwenda mbali zaidi na
kutumia chupa hizo kwa ujenzi, hutumika pia kama mapambo ya ndani,
hujengea uzio wa nyumba, hutumia kujengea paa mahali pa kuhifadhia
magari, hugeuzwa `shamba’ kwa kupanda mimea katika maeneo ya mijini,
lakini wapo wanaojenga pia mabanda ya mifugo, kuwekea miswaki,
kutengeneza maboti na kadhalika.
KUSAMBAZA TEKNOLOJIA
Anasema wako tayari kusambaza teknolojia hiyo kwa watu au taasisi
nyingine, akitolea mfano zipo baadhi ya shule na watu binafsi walioomba
kufundishwa teknolojia hiyo ili waweze kuitumia kwa ujenzi wa majengo
mapya.
ADUI WA MAZINGIRA
Kwa kiasi kikubwa, chupa za plastiki zinapaswa kutumika tena, lakini
sehemu kubwa ya shehena za chupa inaishia kuwa ni taka zinazoendelea
kutupwa na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wengi duniani.
Inaelezwa kuwa kuna mamilioni ya tani za chupa ambazo ziko ardhini,
baharini, kwenye maziwa na mito. Chupa hizi kamwe hazitaoza na
zitaendelea kuwa ni sehemu ya kero na uchafuzi wa mazingira.
Hivyo inaonekana kuna haja kwa serikali kuhakikisha zinafanya
maboresho ya mitandao ya maji, ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na maji
safi na salama katika makazi yao.
Katika nchi zilizoendelea zaidi duniani, matumizi ya maji ya chupa za
plastiki ni makubwa kutokana na kampeni kubwa zinazofanywa na kampuni
zinazozalisha bidhaa ya maji kwa kuwaaminisha kwamba kwa kunywa maji ya
chupa wana uhakika wa maisha na usalama wao, ikilinganishwa na maji
yanayotoka moja kwa moja kwenye bomba
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment