Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Leskar
Sipitieck akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri
ya Wilaya hiyo baada ya kupitisha mpango wa bajeti ya shilingi bilioni
25.3 kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kushoto ni Makamu Mwenyekiti Albert
Msole na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Zuwena Omary na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri hiyo Yefred Myenzi.
MADIWANI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamepitisha
rasimu ya mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 25.3 kwa mwaka wa fedha
wa 2018/2019.
Akizungumza
baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya hiyo, Jackson Sipitieck alisema vipaumbele vya bajeti hiyo ni
elimu, afya, maji na viwanda.
Sipitieck
alisema suala la kupitishwa kwa bajeti ni jambo moja na utekelezaji ni
jambo lingine, hivyo kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake
ipasavyo wakiwemo madiwani na watumishi, ili kufanikisha hilo. Alisema
kila mmoja kwa nafasi yake akisimama kwa nguvu zote, wilaya ya
Simanjiro itapiga hatua kubwa ya maendeleo na wananchi wake watakuwa
wanapata huduma zao za kijamii kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi alisema
bajeti hiyo ni kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ikiwemo miradi ya
maendeleo, ruzuku ya uendeshaji ofisi na mishahara. Myenzi alisema wilaya hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha wanaboresha vipaumbele vyao vya elimu, afya, maji na viwanda. Alisema mazao ya mifugo, ikiwemo maziwa, ngozi na nyama inapaswa kuboreshwa ili iwe chachu ya vichocheo vya uchumi.
Katibu
Tawala wa wilaya ya Simanjiro Zuwena Omary aliwapongeza madiwani wa
halmashauri hiyo kwa kupitisha mpango huo wa bajeti ya mwaka 2018/2019
kwa manufaa ya wananchi. "Pamoja
na hayo tunapaswa kuhakikisha tunatekeleza agizo la kila mkoa kuwa na
viwanda 100 kwa sisi Simanjiro kuanzisha viwanda 15 ambayo vitasambazwa
kwenye kata zetu na vijiji," alisema Omary.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Komolo, Michael Haiyo aliipongeza bajeti hiyo na kusisitiza ikamilishwe kwa vitendo. Haiyo
alisema bajeti hiyo imegawanywa bila upendeleo kwani kata zote
zimepatiwa miradi ila umuhimu wake utaoneka endapo itatekelezwa kwa
vitendo. Diwani
wa kata ya Naisinyai, Kilempu Ole Kinoka alisema bajeti hiyo inapaswa
kujali suala zima la uboreshaji wa mifugo kwani asilimia kubwa ya
wananchi wa eneo hilo ni wafugaji.
"Sisi
kwetu kahawa ya Simanjiro ni mifugo ambayo ni roho ya uchumi, hivyo
tunapaswa kulizingatia hilo kwenye utekelezaji wa bajeti yetu," alisema
Ole Kinoka.
0 comments:
Post a Comment