Home » » ‘GHARAMA KUBWA KIKWAZO CHA KUUNGANISHA HUDUMA YA UMEME’

‘GHARAMA KUBWA KIKWAZO CHA KUUNGANISHA HUDUMA YA UMEME’

Na Yusuf Dai, Manyara
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema moja ya vikwazo vinavyokwamisha jitihada za Serikali za kuhakikisha huduma ya umeme, inawafikia wananchi wengi zaidi ni gharama za kuungunisha umeme.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akizungumza na wadau wa nishati na madini.

Alisema gharama hizo zimekuwa ni kikwazo katika azma ya Serikali ya kutimiza lengo la asilimia 30 ya wananchi kuunganishiwa umeme ifikapo mwaka 2015.

Aidha, alisema kwa kuzingatia changamoto hizo, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imedhamiria kupunguza gharama za kuunganishwa umeme wa njia moja kwa wateja wadogo mjini na vijijini kwa wastani wa kati ya asilimia 30 na asilimia 77.

Alisema kwa kufanya hivyo wateja wengi watamudu gharama na hatimaye kuongeza kasi ya kuunganisha umeme na kutokana na uamuzi huo gharama za umeme zimepungua tofauti na awali.

Alisema wateja watakaojengewa njia katika umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo maeneo ya vijini wataunganishwa kwa Sh 177,000 sawa na asilimia 61.11ambapo kwa upande wa mijini wataunganishiwa kwa Sh 320,960 sawa na asilimia 29.48.

Alisema viwango hivyo vitaanza kutumika Januari, 2013 na Serikali imeanzisha utaratibu wa kugharamia miundombinu ya kuwafikishia umeme wateja kwa miradi inayopata ruzuku.

“Mpango huo utapunguza gharama za kuunganishiwa umeme kwa wastani wa asilimia 80, kulingana na idadi ya nguzo na mfumo utakaotumika yaani single au three phase, ambapo idadi ya wateja wa awali wataunganishiwa umeme kupitia mpango huo kwa shilingi 100,000,” alisema Profesa Muhongo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa