na Mwandishi wetu, Karatu
WAKULIMA wa shayiri wameombwa kuwatumia na kusikiliza ushauri wa wataalamu wa kanda.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Meneja wa Kiwanda cha kuzalisha
kimea cha Moshi, Vitus Muhusi, katika maonesho ya wakulima wa shayiri
yaliyofanyika Kijiji cha Njia panda getini wilayani Karatu, mkoani
Arusha.
Muhusi alisema utaratibu uliopo ni kwamba wakulima hao wanasaidiwa
pembejeo, elimu na mafunzo bure kutoka kwa wataalamu washauri wa Kampuni
ya Bia nchini (TBL), hivyo hawana budi kutumia fursa hiyo ya kipekee
kwao.
“Wataalamu wetu wanajua katika kipindi hiki ili mkulima aweze kupata
mazao yenye tija kwa mazingira haya yenye mabadiliko ya tabia nchi
kwamba mkulima anatakiwa kufanya nini na nini,” alisema.
Katika maonesho hayo, Muhusi alibainisha kuwa kiwanda cha kuzalisha
kimea kinahitaji tani takriban 15,000 za shayiri kwa mwaka ili
kutosheleza mahitaji, hatua ambayo wakulima bado hawajaifikia.
Naye mkulima wa Shayiri kutoka Kijiji cha Rotia Kati, Anatoly Lohay,
alisema ana ujasiri wa kulima kiasi cha ekari 200 kutokana na
kuhakikishiwa soko na TBL.
“Naiomba TBL waendelee kusaidia wakulima ili waweze kuthubutu kufungua
mashamba mapya zaidi,” alisema Lohay ambaye ana mpango wa kuanzisha
mashamba mengine wilayani Sumbawanga.
CHANZO: DAIMA
0 comments:
Post a Comment