na David Frank, Simanjiro
WAKAZI wa mji mdogo wa Mererani,
wilayani Simanjiro, Manyara, wameafiki utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa
barabara kwa kiwango cha lami utakaogharimu sh bilioni 26 ambao utajenga
barabara ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi Mererani.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi baada ya
wakazi hao kupiga kura ili kubaini wanaopinga ujenzi huo uliopitishwa na
serikali katika bajeti yake ya 2012/2013, ambapo ilionesha idadi kubwa ya
wakazi wa mji huo wanaafiki mradi huo.
Akizungumza katika mkutano huo,
Kaimu Katibu, wa mamlaka ya mji mdogo huo, Edmund Tibiita, alisema utekelezaji
wa mradi huo wa kilomita 27 zitakamilika katika kipindi cha miezi 18.
Alisema kukamilika kwa barabara hiyo
kutafanikisha kuunganisha mikoa ya Kilimanjaro na Arusha pamoja na mikoa
mingine ya jirani ambapo utasaidia kuendeleza mji huo, ikiwa ni sambamba na
eneo la viwanda (EPZA) litakalojengwa Manyara.
Alisema kuwapo kwa miradi hiyo
kutasaidia upatikanaji wa ajira ambapo mkandarasi amekubali kutoa nafasi za
ajira zipatazo 300 kwa wakazi wa mji mdogo.
Akizungumzia suala la ulipaji fidia
alisema kutokana na barabara hiyo kupanda hadhi ya wilaya hadi mkoa na
kumilikiwa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), hivyo serikali italipa
fidia kwa wale waliojenga umbali wa kuanzia mita 15 hadi 30.
Naye Diwani wa Kata ya Mererani, Justine Nyari,
aliwataka wakazi hao kukubali changamoto zilizopo ili kurahisisha shughuli za
maendeleo kufanyika kwa wakati, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi
mbalimbali.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment