Home »
» Hamashauri Babati yabomoa nyumba za NHC
Hamashauri Babati yabomoa nyumba za NHC
|
|
HALMASHAURI ya Mji wa Babati imebomoa nyumba za Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) zipatazo 52 zilizojengwa katikati ya mji kwa
ajili ya kupisha eneo hilo kuwa kituo cha biashara kwa wawekezaji.
Akizungumza wakati wa ubomaji nyumba hizo jana, Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo, Omary Mkombole, alisema eneo hilo kwa sasa
linahitajika kwa matumizi mengine na pia nyumba hizo zimeshakuwa
chakavu, hivyo zinaweza kuleta madhara kwa wananchi.
“Huu mji kwa sasa unakua na maendeleo yanahitajika zaidi, hivyo basi
hatuna budi kuendeleza mji kwa manufaa ya wananchi, na kubomoa nyumba
hizi haimaanishi tunawaonea ila ni mpango mkakati wa muda mrefu,”
alisema Mkombole.
Alieleza awali walitoa taarifa kwa wamiliki wa nyumba hizo ambao
hawakukubaliana na taarifa hizo, hivyo kuamua kupeleka shauri lao
Baraza la Nyumba na Makazi wilayani Babati ambako shauri hilo lilitupwa
na kupewa siku 90 za kuhama.
Aidha, alisema baada ya siku walizopewa kuisha, wamiliki hao waliomba
kuongezewa muda ambapo halmashauri iliwaongezea siku 30.
“Wapangaji waliokuwa wanakaa hapa hatukuwa tukichukua kodi zao na
tulisimamisha zoezi hilo tangu mwaka 2010 baada ya kuwatangazia kuhusu
kubomoa nyumba hizi na sababu zake,” alifafanua mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, alisema halmashauri itatoa viwanja kwa kuwauzia wale
wasiopata viwanja na kuongeza kuwa kuna viwanja 20,000 kwa ajili ya
makazi.
Wamiliki wa nyumba hizo walidai halmashauri haijawatendea haki,
kwani muda waliopewa kuhama na kupisha eneo hilo ulikuwa mdogo, hivyo
wengine kuamua kupanga huku wengine wakikosa mahali pa kuhamia.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment