Home »
» MJUMITA waomba wataalamu wa misitu
MJUMITA waomba wataalamu wa misitu
|
|
WANACHAMA wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania
(MJUMITA) Kata ya Bonga, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wameiomba
serikali kuwapelekea wataalamu wa misitu wakapime msitu wao ili uweze
kuingia kwenye orodha ya misitu shirikishi.
Rai hiyo wameitoa jana kwenye mkutano wa kushirikishana juu ya hali
ya utawala bora wa misitu iliyowashirikisha wanamtandao hao na wadau
wengine wa misitu.
Wanamtandao hao walisema wanahitaji wataalamu wa kupima msitu huo kwa
kuwa bado wana changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na migogoro
ya mipaka kati ya vijiji na mitaa, motisha kwa walinzi unaosababisha
uharibifu mdogo mdogo ndani ya msitu pamoja na kutokuwa na mfuko wa
kuendeshea shughuli za msitu huo.
“Sisi wanamtandao wa Kata ya Bonga tunaomba wataalamu waje wapime
msitu ili tuweze kuingia kwenye orodha ya misitu shirikishi jamii/
Tanzania na pia tupatiwe rangi kwa ajili ya kuweka mipaka inayozunguka
jamii," walisema wana mtandao hao.
Aidha, walibainisha kwamba pamoja na changamoto walizonazo, kupitia
msitu huo wameweza kupata elimu juu ya kuhifadhi mazingira na kutunza
misitu.
Kwa upande wake Mratibu wa (MJUMITA) Kanda ya kati, John Reuben,
alisema ili mitandao mingi iweze kufanya vizuri kwenye utunzaji wa
misitu na kufanya rasilimali hizo kutumika kwa manufaa ya jamii yote,
wanahitaji kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa vijiji na jamii
nzima.
Reuben alibainisha kwamba lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa
huduma zinazotokana na misitu zinahifadhiwa kwa manufaa ya jamii.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment