WATU wanne wamefariki na 32 kujeruhiwa baada ya basi la abiria la
Polepole, trekta na bajaji kugongana eneo la Makatanini, wilaya ya
Babati mkoa wa Manyara.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mussa Marambo, akizungumza na wanahabari jana
kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa Akili Mpwapwa alisema ajali
hiyo ilitokea Desemba 7 majira ya saa mbili usiku.
Marambo alieleza chanzo cha ajali hiyo ni trekta kuegeshwa katikati
ya barabara bila alama, ndipo basi la abiria lenye namba T 898 BKN aina
ya fusso, mali ya Issack Polepole likagongana na trekta aina ya Swaraj
lililokuwa halina namba za usajili, huku likiendeshwa na Clement Tuji.
Waliokufa katika ajali hiyo ni Shaibu Olae (25), Mwalimu wa Sekondari
Aldersgate Nicodemu Mofuru (27) mkazi wa majengo mapya, Charles Exaud
na mwanamke mmoja ambaye hakuweza kufahamika jina lake.
Wakati huohuo waendesha pikipiki wilayani Kiteto maarufu bodaboda
wamechoma nyumba ya Mosses Lucas (35) mkulima wa Kibaya wakimtuhumu kwa
mauaji ya dereva mwenzao Rasuli Yahaya (17) mkazi wa mafichoni Kijiji
cha Mbeli.
Kamanda Marambo alisema tukio hilo limetokea eneo la Ngarenaro Desemba 4 majira ya saa saba mchana.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini walioshiriki na kusababisha mauaji hayo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment