DIWANI wa Ganana katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, mkoani
Manyara, Zakayo Tarmo, amemkana mtendaji wake wa kata na kukataa
kusomewa taarifa ya maendeleo akimtuhumu hampi ushirikiano katika
utendaji ndani ya kata hiyo.
Diwani huyo alitoa shutuma hiyo mbele ya kikao cha baraza la madiwani
wakati watendaji wakitoa taarifa za kata zao kwa niaba ya madiwani wao
ambapo ilipofika zamu yake alisimama na kutaka taarifa ya kata yake
isisomwe kwa kuwa haikuwa sahihi.
Tarmo alieleza mtendaji wa kata yake hakuwa mtendaji bali ni mtawala
ambaye anafanya kazi zake bila kutoa ushirikiano kwa diwani wake na
kufanya shughuli za maendeleo ya kata hiyo kwa njia anazojua mwenyewe
bila kuitisha vikao.
“Huyu mtendaji mliyeniletea ndani ya kata yangu ni mtawala
anayeendesha shughuli kibabe na bila kunipa mimi diwani wake
ushirikiano wowote, sijui kwa sababu mimi ni CHADEMA, au kwa kuwa mimi
si CCM.
“Hiyo taarifa anayotaka kuisoma ameiandaa na nani na ameiandalia wapi
mimi sijui, kwa hiyo taarifa hiyo si sahihi na wala siitambui,”
alisisitiza Tarmo.
Kwa upande wake mtendaji aliyetuhumiwa, Grace Dofa, hakuweza
kuzungumzia shutuma hizo zaidi ya kutoa lawama juu ya diwani wake
kwamba anafanya vurugu ndani ya kata hiyo na kusababisha wananchi
kumchukia na yeye kufanya chuki juu yake.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Felix Mabula,
alichukua nafasi yake na kumtaka mtendaji huyo kusoma taarifa
aliyoiandaa kwa heshima ya kikao na kutaka suala hilo kuzungumziwa
wakati wa majadiliano.
Mabula alibainisha kuwa wanajipanga kufanya uchunguzi wa kina juu ya shutuma hizo ili kubaini mapungufu ya mtendaji huyo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment