Home » » Naibu Spika ashitakiwa kwa PM adaiwa kuchochea mgogoro Kiteto

Naibu Spika ashitakiwa kwa PM adaiwa kuchochea mgogoro Kiteto

Naibu Spika Job Ndugai
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kiteto, Mainge Lemalali, amemshtaki Naibu Spika Job Ndugai kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda akimwelezea kuwa ndiyo anachochea mgogoro kati ya wakulima na wafagaji wilayani hapa ambapo watu takriban 15 wameuawa.
 
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Lemalali alisema halmashauri yake ililazimika kuwasilisha mashtaka dhidi ya Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, kwa Waziri Mkuu Pinda wakati alipotembelea hapa juzi kuwapa pole kufuatia mauaji na vurugu zilizotokea kati ya wakulima na wafugaji na pia kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
 
“Ni kweli tumemweleza Waziri Mkuu alipofika hapa kuwa mgogoro huu unachochewa na Ndugai kwa kutamka hadharani akiwataka wakulima kutoka nje ya wilaya hii (Kongwa, Kibaigwa) kuja huku kulima kwenye maeneo ambayo mahakama imepiga marufuku,” alisema.
 
Alisema Mahakama ya Rufani katika hukumu iliyotolewa mwaka 2012, iliwapa ushindi halmashauri dhidi ya wakulima 50 matajiri waliokuwa wakihodhi maeneo makubwa na kuendesha shughuli za kilimo katika Hifadhi ya Jamii ya Emborei ya Murtangosi, inayomilikiwa na vijiji saba.
 
“Tatizo langu mimi hapa ni kusimamia hii kesi hadi tumepata ushindi,
ndio naona Ndugai na wenzake wananichukia.
 
“Suala la kesi ni kweli Ndugai lazima anilaumu mimi, manake ningelegalega tu wenyeji wanaoishi katika vijiji hivyo wangepata ardhi kwa malisho ya mifugo yao na kilimo.
“Ndugai anashindwa kusimamia sheria na anachofanya ni uchochezi ambao
hauna misingi,” alisema.
 
Alisema Ndugai kama Mbunge na Naibu Spika ni mtu mkubwa lakini hata yeye (Mwenyekiti wa Halmashauri pia ni mtu mkubwa katika eneo la alilopewa kulisimamia kwa mujibu wa sheria.
 
“Ndugai amekuwa mtu wa kupamba majukwaa kwa kuhamasisha na kuchochea mgogoro huu kwa kuwa wengi waliovamia eneo hilo la hifadhi ni wapiga kura wake kutoka Kongwa hivyo ana maslahi binafsi mgogoro huu,”alisema na kuongeza wengine wanatoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa
Dodoma.
 
Hata hivyo, alisema watu wanaotaka kuhamia wilayani humo na kuendesha shughuli za kilimo hawazuiwi alimradi tu wanafuata sheria kwani Katiba ya nchi inasema kila mtu ana haki ya kuishi po pote pale mradi tu havunji sheria.
 
“Sasa hivi hali ya wilaya imekuwa tete kutokana na uchochozi wa Ndugai, yeye ni kiongozi wa kitaifa anayeshiriki kutunga sheria hivyo hakupaswa kuhamasisha watu majukwaani,” alisema.
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbula, alisema anashangazwa na hatua ya mbunge mwenzake (Ndugai) kumshambulia hadhari na akahoji uchungu wa mbunge huyo na kama ana maslahi gani katika mgogoro huo.
 
“Siwalaumu sana kwa sababu wanasiasa tunajuana uwezo wetu, huyu Ndugaiana maslahi gani kwa wilaya ambayo siyo yake.
 
“Hatujafanya utafiti ni lipi hasa kinachompa msukumo huo, bado ninatafakari na tutazijua sababu hizo hapo baadaye,” alisema.
 
Ndugai amekuwa akisikika kutoa matamko dhidi ya Mkuu wa Wilaya Umbula tangu mgogoro kati ya wafugaji na wakulima ulipozuka tena hivi karibuni akimtaka aachie ngazi wadhifa wake kwa madai ya kushindwa kuutafutia ufumbuzi.
 
Amekuwa akifanya hivyo maeneo mbalimbali jimboni kwake Kongwa katika majukwaa au wakati akishiriki mazishi ya watu waliouawa kwenye mapigano hayo.
 
Akizungumzia hali ya amani na utulivu kwa sasa, Umbula alisema makamishna wawili wa polisi kutoka makao makuu Dar es Salaam wapo wilayani hapa kuchunguza pamoja na mambo mengine watu wanaotuhumiwa kufanya mauaji.
 
Alisema wilaya yake bado inasisitiza agizo la Waziri Mkuu Pinda alilolitoa juzi katika mkutano wake wa hadhara wilayani hapa ikiwa ni utekelezaji wa amri ya mahakama ya kuwataka waliovamia hifadhi hiyo waondoke.
 
Alisema wilaya itawapatia usafiri wale watakaoshindwa kuhama na chakula wale ambao vyakula vyao vilichomwa moto katika mapigano hayo.
 
Chadema yamshauri Rais awafukuze kazi DC na DED
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kutokana na mgogoro mkubwa wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji unaoendelea wilayani Kiteto ambao umefikia hatua ya kusababisha maafa makubwa ya umwagikaji wa damu, mauaji ya watu na uharibifu wa mali, Wizara Kivuli, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imemshauri Waziri Mkuu Pinda achukue hatua za kinidhamu kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Martha Umbulla na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Jane Mutagurwa, kisha amshauri Rais Jakaya Kikwete awafute kazi wote wawili mara moja.
 
Waziri Kivuli, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), David Silinde, katika taarifa yake amesema Waziri Mkuu anapaswa kumshauri rais amfukuze kazi DC Umbulla kwa sababu akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto, amezembea kuwajibika ipasavyo na kusababisha kukosekana kwa usalama wa raia na mali zao katika eneo hilo, hadi kutokea kwa umwagikaji wa damu na mauaji makubwa.
 
Aidha,  Waziri Mkuu Pinda  achukue hatua za kinidhamu na kumshauri Rais Kikwete amfukuze kazi Mkurugenzi wa Wilaya Jane Mutagurwa, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa halmashauri, kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo kuweka mipango bora ya  mgawanyo wa ardhi kwa matumizi mbalimbali kwa wananchi wa eneo husika, hali ambayo ingeweza kuepusha maafa hayo.
 
Baada ya mahakama kutoa amri ya wananchi hao kuhama, uongozi huo wa wilaya ulipaswa kuweka mipango ya kusaidia kupatikana ardhi nyingine kwa ajili ya wananchi hao kuhamia. 
 
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa