Home » » Watatu wasakwa kwa kuua faru hifadhi ya Serengeti

Watatu wasakwa kwa kuua faru hifadhi ya Serengeti

  Serikali kuchukua maazimio ya Kamati ya Lembeli
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama inawasaka watu watatu wanaodaiwa kuwa majangili akiwemo mwanamke baada ya kumuua faru kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Manyara na kutoweka na pembe zake.
 
Kadhalika, alisema majangili hao waliingia kwenye mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kuvamia basi la abiria juzi majira ya saa 9:00 alasiri na kuwapora wasafiri fedha na mali.
Nyalandu alitoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kuhusu hali ya ujangili na mkakati wa serikali katika kupambana nao.
 
Alisema serikali katika kutekeleza maazimio ya bunge yaliyotokana na kamati ya James Lembeli, imechukua hatua mahususi ya Rais Dk. Jakaya Kikwete ya kuunda tume ya kimahakama kwa ajili ya kuchunguza tuhuma zilizotolewa dhidi ya Operesheni Tokomeza Majangili.
 
“Tunasikitika sana na taarifa tulizozipata usiku wa kuamkia leo (jana) majangili watatu akiwemo mwakamke mmoja walimuua faru katika eneo la Moru, kusini mwa hifadhi ya Serengeti baada ya askari wa wanyama pori waliokuwa doria kugundua mauaji hayo na pembe zake zilikuwa zimetolewa,” alisema na kuongeza kuwa.
 
“Serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge yaliyotolewa na Kamati ya Lembeli imechukua hatua mahususi na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na msako wa kuwasaka na kukabiliana na majangili,” alisema Nyalandu.
 
Akijibu madai ya dhumuni la  mkutano wake na kamati ya ulinzi na usalama za mikoa ya Dodoma na Manyara, alisema mkutano huo ulihusisha wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo vya usalama kujadili migogoro ya mipaka baina ya hifadhi ya Tarangire, pori la akiba la Mkungunero na wananchi.
 
Akifafanua alisema miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na Operesheni Tokomeza  inayotarajiwa kuanza kwa awamu ya pili.
 
Alisema serikali imeanza kutekeleza maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Lembeli na agizo la rais la kuundwa Tume ya Kimahakama ili kubaini ukweli wa tuhuma zilizojitokeza.
 
“Hali ya ujangili nchini ni mbaya na kwa namna yoyote serikali itapambana na vitendo hivi vya ujangili na uhujumu uchumi vinavyofanywa dhidi ya raslimali za Taifa,” alisema.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi  kwa njia ya simu, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Eraston Mbwilo, alisema kwa sasa hali imetulia na kwamba wananchi wanaondoka kwenye maeneo hayo katika hali ya utulivu.
 
“Wananchi wanaondoka kwa utulivu na amani imechu
kua nafasi yake, polisi wanaendelea na kuimarisha ulinzi na usalama wa raia,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mkutano kati yao na Naibu Waziri Nyalandu, alisema walijadili kuhusu awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza majangili jinsi itakavyoimarishwa.
 
“Mheshimiwa Nyalandu alisisitiza ushirikiano katika operesheni ijayo na alizijulisha kamati za ulinzi za mikoa yetu (Manyara na Dodoma)… lakini cha ajabu nimesikitishwa na taarifa za uongo zilizozagaa kwamba Nyalandu alikashifu na kuishambulia kamati ya Lembeli” alisema na kuongeza kuwa.
 
“Nashukuru wewe mwandishi, umepiga simu kutaka kujua hali ya usalama na nini kilitokea kwenye mkutano wetu… tulijadili mambo makuu matatu, kuanza kwa operesheni awamu ya pili, serikali kutekeleza maagizo ya kamati ya bunge na agizo la rais kuunda tume ya kimahakama ili kubaini ukweli wa tuhuma zilizojitokeza” alisema Mkuu wa Mkoa Mbwilo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa