Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
Kauli hiyo aliitoa katika mazishi ya Mchungaji Emmanuel Manyaji, pamoja na mwanaye, Shukuru Manyaji, waliouawa kinyama katika mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani humo.
Alisema mgogoro wa Kiteto ni wa muda mrefu hivyo anashangazwa na kauli za viongozi wilayani humo kudai kuwa ni mapigano ya wakulima na wafugaji wakati wanaouawa kule ni wakulima.
Ndugai alisema kinachoendelea Kiteto ni mauaji ya kikabila, ambayo yamejengwa na viongozi katika wilaya hiyo.
“Mimi nashangazwa mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na watu wanauawa kinyama kule kama vile hakuna viongozi, na wanaofanya mauaji kuna jeshi limekodiwa kwa ajili ya kuwaondoa wakulima,” alisema Ndugai.
Aidha, alibainisha kuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kiteto alitamka wazi kuwa watawaua watu wa Ndugai na ajiandae kuchukua maiti wake.
“DC na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa mnasubiri nini kujiuzulu, jamani hamfai kuwapo kwani hamlindi raia na mali zao na mauaji haya yanatokea hata hakuna mtu anayekamatwa kwanini sasa nyie mpo?” alihoji Ndugai.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Martha Umbulla, kujiuzulu na kubaki na nafasi yake ya ubunge wa Viti Maalum maana ukuu wa wilaya umemshinda.
Naye Mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Dodoma, Hezekiah Chibulunje, alikemea mauaji hayo na kusema kuwa hiyo siyo Tanzania anayoifahamu.
Chibulunje alisema mgogoro wa Kiteto umelenga kundi moja na una hila ndani yake na kuitaka serikali kulipa uzito mkubwa suala hilo maana watu wanazidi kupoteza maisha kila uchao.
Mchungaji wa Kanisa la LPIA Kiteto, Chilauni Richard, alisema yeye ni rafiki wa karibu ya Mchungaji Manyaji na siku ya tukio alipitia nyumbani kwake akiwa na mwanaye wakienda kanisani kusali.
Alisema mauaji hayo ni ya kikatili na inawezekana Kiteto siyo sehemu ya Tanzania, ambayo inasifika kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu.
Aliitaka serikali kuunda tume huru, ambayo itasaidia kutafuta suluhu ya tatizo hilo kwani watu wamepoteza maisha na mali zao.
Chadema yaitaka serikali kuwajibika
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka serikali kusitisha operesheni inayoendelea katika eneo lenye mgogoro wa wakulima na wafugaji, kila upande ukidai haki yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Waziri Kivuli wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili, ni wakati wa serikali ya CCM kupitia kwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, ijitafakari.
Alisema kutafakari huko kujikite katika uwezo wake wa kushughulikia viini vya matatizo kwa uharaka, umakini na usahihi badala ya kuwa mabingwa wa kushughulika na matokeo ya tatizo wakiwa wamechelewa.
“Kutokana na hayo ambayo yameshatokea Kiteto hadi sasa, damu za watu zimemwagika katika suala ambalo lilipaswa kuwa limeshapatiwa ufumbuzi kama serikali ingelikuwa inazingatia uwajibikaji kwa wananchi wake, tunamtaka Waziri Chiza kuwajibika,” alisema.
Aidha, aliishauri Kamati Teule ya Bunge inayoendelea na kazi yake ya kuchunguza migogoro huo kufanya kazi hiyo kwa umakini na usahihi ili kubaini kwa uhakika viini vya migogoro husika ili bunge kwa niaba ya wananchi lipate majawabu sahihi yatakayomaliza migogoro ili wakulima na wafugaji wapate haki zao na waendelee kuishi kwa amani kwa kutimiza wajibu wao kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
CUF YAMTAKA DC AJIUZULU
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani mauaji hayo na kuitaka serikali kutoyachukulia maisha ya binadamu kama kitu cha kuchezea.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Haki za Binadamu wa CUF, Abdul Kambaya, mgogoro huo umedumu kwa miaka minne sasa bila kuchukuliwa hatua zozote.
“Utaratibu wa serikali wa matumizi ya ardhi bila ushiriki wa wazi kwa wananchi umekuwa chanzo cha migogoro mingi ya ardhi nchini Tanzania,” alisema.
Alisema mara nyingi serikali ya CCM imekuwa ikiziangalia chokochoko hizo na kuziacha bila ufumbuzi wa kudumu huku sheria zinavunjwa bila hatua kuchukuliwa na matokeo yake ni mauaji yanayoendelea Kiteto.
Aidha, walimtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Umbulla, kujiuzulu kutokana na kushindwa kutatua mgogoro huo hadi mauaji ya kutisha yamejitokeza.
PINDA ASHINDWA KUTOKEA
Mamia ya watu ambao walifika wilayani Kiteto jana kwa ajili ya kumsikiliza uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu mgogoro wa Hifadhi ya Embroi Murtangosi walilazimika kuondoka baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa hadhara.
NIPASHE lilishuhudia watu wakiwa wanamiminika kwenye mji kwa Kibaya kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa Pinda.
Mweka Hazina wa Chama cha Wafugaji na Wakulima Wilaya ya Kiteto (Chawaka), Abdul Mussa, alisema watu walifika katika makao makuu ya wilaya hiyo ya Kibaya kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa hadhara, lakini walilazimika kuondoka baada ya kuelezwa kuwa Pinda hataweza kufika tena.
Mbali na Pinda kushindwa kufika, zoezi la kuwakamata watu waliohusika katika mapigano hayo yaliyosababisha vifo vya watu 18 hadi sasa, limekuwa gumu kutokana na wanahusika kujificha.
Habari kutoka hifadhi ya Murtangosi zilisema kuwa kikosi cha polisi kikiongozwa na Kamishna wa Operesheni wa Polisi, Simon Sirro, kimewasili katika hifadhi hiyo.
Umbulla, alisema wanasubiri ripoti ya wapelelezi ingawa watu wanaofanya mauji hayo wanahofiwa kutoka nje ya Kiteto.
Akizungumzia ziara ya Waziri Mkuu, Pinda, alisema alitarajiwa kufika jana, lakini ziara hiyo iliahirishwa hadi leo kutokana na kutingwa na majukumu mengine.
Mgogoro huo ulioanza mwaka 2006, unatokana na wafugaji na
wakulima kugombea ardhi kwenye eneo la hifadhi ya hiyo.
Mapigano kati ya pande hizo mbili hizo mbili yamesababisha vifo vya watu 18 na wengine 14 kujeruhiwa.
Imeandikwa na Augusta Njoji, Kongwa; Jacqueline Massano na Salome Kitomari, Dar.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment