Kiteto:Bahati ni kweli ana bahati kama jina
lake lilivyo Bahati. Katika mapigano, yaliyotokea hivi Karibuni, mtoto,
Bahati Juma alikuwa ni mmoja wa watu waliojikuta wako katikati ya
mapigano hayo.
Mtoto huyu anasema alikamatwa na kundi la wafugaji
wa Kimasai, akiwa ndani ya nyumba yao iliyochomwa moto. Katika tukio
hilo, Bahati alinusurika kufa ingawa tayari sime ilikuwa imeanza kukata
shingo yake.
Hivi sasa Bahati amelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, akiuguza jeraha la kukatwa na sime na
ameshonwa nyuzi nane huku akiwa na majeraha ya fimbo mgongoni na
mikononi.
Ndugu zake watatu ambao ni wakulima wote kutoka
mkoani Dodoma, wameuawa ambao ni Juma Mlangwa (47) na Yohana Hivo (33)
waliuawa papohapo na Mussa Juma alifariki akiwa hospitali.
Katika mapigano hayo yaliyotokea Desemba 21 Kijiji
cha Olpopong, wakulima wengine wanane walijeruhiwa, mmoja alikuwa
mahututi. Mussa Juma ambaye alichomwa mkuki wa mbavu, alihamishiwa
hospitali ya Mkoa ya Dodoma, alifariki baadaye.
Wengine waliolazwa hospitali ya wilaya ya Kiteto
ni Emanuel Mathias (26), Hoti Damas (38), Mwajuma Hamis (20), Habiba
Ally(16 ) na Mwajuma Martin(33).
Daktari azungumza
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Kiteto, Thomas Ndalio anasema, hali za majeruhi hao saba zinaendelea vizuri.
“Mussa ndio hali yake ilikuwa mbaya sana na ndio
sababu alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu zaidi, kwa
bahati mbaya alifariki,”anasema Dk Ndalio.
Bahati asimulia alivyonusurika kifo
Anasema, anakumbuka Desemba 21 alikuwa nyumbani na ndugu zake, wakiwa wamepumzika baada ya kutoka shamba kulima.
Siku hiyo anakumbuka kulikuwa kumezuka mgogoro
katika eneo la malisho kati ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Kimasai.
Wafugaji hao walikuwa wameingiza katika mashamba yao, mifugo na
walifanikiwa kuwafukuza.
Hata hivyo, anasema ilionekana wafugaji hao, walikasirishwa na kufukuzwa lakini waliondoka na hasira.
“Sasa mimi nikiwa ndani ghafla nilisikia nje watu
wakisema kuna vita! kuna vita!. Nilipotaka kutoka, tayari nyumba yetu
ilikuwa imeshika moto,” anasema Bahati.
Anasema aliamua kutoka mbio ili kujiokoa, lakini
alijikuta yuko mikononi mwa wafugaji wa kimasai, walimkamata na kuanza
kumkata na sime huku wengine wakimchapa.
“Wakati wanaendelea kutaka kunichinja ndugu zangu
wengine walijitokeza, ugomvi ulikuwa mkubwa na hapo niliona wenzangu
wawili wakiuawa kwa kuchomwa mikuki na kukatwa sime”anasema Bahati.
Anasema baada ya tukio hilo, wafugaji waliendelea kuchoma nyumba zao, baadaye wakaondoka huku wakionya wasisumbuliwe.
“Wakati huo mimi nilikuwa chini nalia, damu
zilikuwa zinanivuja, baadaye nilichukuliwa na kuletwa hapa
hospitalini,”anasema Bahati huku akisisitiza kuwa Serikali ikomeshe
haraka mgogoro huo.
Aomba Serikali kumaliza mgogoro
Bahati anaomba Serikali, kutatua mgogoro wa ardhi
katika wilaya hiyo, kwani hali ya usalama sio nzuri katika kijiji cha
Olpopong wanachoishi.
“Tunaomba tu watusaidie tukae kwa amani na hawa wafugaji,“anasema Bahati kwa uchungu.
Anasema kama amani ikipatikana katika eneo lao,
atarejea kuishi, lakini kwa sasa bado ana hofu kwani bado hajui ndugu
zake wengine wamekimbilia wapi.
Chanzo cha mapigano
Saitoti Kalanga, ni Mwenyekiti wa Kijiji cha
Olpopong kilichotokea mapigano baina ya wakulima na wafugaji na
kusababisha vifo vya watu wawili, anasema chanzo cha mapigano hayo ni
watu kuvamia ardhi ya kijiji bila kufuata mpango wa matumizi bora ya
ardhi na kila wanapotakiwa kuondoka wamegoma.
Anasema watu hao wakiwemo wakulima wamejianzishia vitongoji
batili ndani ya kijiji. Katika maeneo wanayolima wamekuwa wakikamata
mifugo inayopita na kuikatakata kwa mapanga jambo ambalo limekuwa kero
kubwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
“Wakulima ni wavamizi, hawatambui Serikali ya
kijiji, wameingia tu kwa nguvu na wanalima kwa kukata miti ovyo jambo
ambalo limewaudhi wafugaji,”anasema Kalanga.
Kalanga anasema kijiji hicho, kilichosajiliwa
mwaka 1993, kina mpango wa matumizi ya ardhi, uliopitishwa na
halmashauri tangu mwaka 2010, lakini umekuwa haufuatwi baada ya wakulima
kuvamia.
Mwenyekiti huyo anaonyesha ramani ya mpango wa
matumizi ya ardhi katika kijiji hicho; ekari 2880 zilitengwa kwa kilimo,
hekari 1, 450 kwa makazi, ekari 9184 kwa malisho na ekari 9805 hifadhi
ya jamii.
“Hivi sasa ardhi ya malisho na hifadhi imevamiwa
na wakulima kutoka Mkoa wa Dodoma, ndiyo sababu kumeibuka
mapigano,”anasema Kalanga.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Eseriani, ambacho
mapigano yametokea, Mariam Ijumaa, anasema kumekuwepo na uvamizi wa
wakulima katika kitongoji chake, anaamini suluhu ni kuwagawia ardhi.
“Uvamizi unaongezeka na hawa wanaokuja hawataki
hata kutambua Serikali ya kijiji, wameanzisha vitongoji vyao
porini,”anasema Ijumaa.
Waeleza suluhu ya mgogoro huo
Saitoti Kalanga, Mariam Ijumaa na Alaisi Nangoro,
wakazi wa eneo hilo wanasema suluhu ya mgogoro ulioibuka katika kijiji
hicho ni kufuatwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Nangoro anasema kwa kuwa tayari kijiji hicho
kilipimwa, ni busara Serikali ikasaidia kufuatwa mpango halali; kama
kuna wakazi wasio na ardhi wapewe.
“Tunapaswa kuishi kwa amani, mapigano yaliyozuka
hapa yasitokee tena, ni muhimu kuheshimu mamlaka za vijiji kwa wale
wanaotaka ardhi,”anasema Nangoro. na mkazi wa kijiji hicho,
Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo, anaeleza Serikali
kusikitishwa na hali ya mapigano ya ardhi katika wilaya ya Kiteto na
hadi kufikia watu watatu kufariki ndani ya wiki moja na wengine wanane
kujeruhiwa.
Mbwilo anaagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto
kusaidia vijiji kuondokana na mapigano ikiwamo kupanga matumizi bora ya
ardhi na kuwaondoa wavamizi. “Haiwezekani watu wavamie tu ardhi kama
hakuna viongozi, ni lazima tufuate sheria,” anasema.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment