Home » » Wakazi Babati na hofu magonjwa ya matumbo

Wakazi Babati na hofu magonjwa ya matumbo

HALI ya usafi katika maeneo kadhaa mjini Babati mkoani Manyara si ya kuridhisha kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wakazi wake.
Wakazi hawa hutupa takataka ovyo kwenye maeneo ya wazi na pembezoni mwa nyumba wanazoishi.
Bila kujali milipuko ya magonjwa na hata athari kwa watoto wanaopita au kucheza katika maeneo hayo, wamekuwa wakitupa takataka huku zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mifuko ya plastiki na kusababisha maeneo ya mji kuzagaa mifuko hiyo.
Baadhi ya wakazi wanaoishi mjini hapa wametoa kero zao huku wakiitupia lawama Halmashauri ya Mji kwa kutokuwa makini na suala zima la utunzaji wa mazingira.
Wakazi hawa wanasema hakuna gari la kubebea takataka ndani ya mji jambo ambalo wamelizungumzia kuwa ni kuhatarisha afya zao.
“Yaani hapa kwa sasa ni kusubiria hayo magonjwa ya mlipuko tu kwani takataka zinazotupwa nyingine zimeoza na zinatoa harufu mbaya, watu bila kujali afya zao na watoto wao wamekuwa wakitupa taka na zinazagaa ovyo hadi sehemu za kuchezea watoto na kupumzikia.
“Tatizo halmashauri yetu inafanya mzaha na afya zetu, tunaweka takataka ndani kusubiria gari la kubebea taka lipite, lakini matokeo yake tunakaa nazo mwezi mzima.
“Siku likipita wanaanza kudai pesa na kama huna hawachukui takataka, hiyo biashara waliyoianzisha wanataka kutuletea maradhi tu,” anasema mama Angel.
Anasema kwamba chanzo cha watu kutupa takataka ovyo ni kutokuwa na gari maalumu na jalala kubwa la kutupia taka.
“Zamani jalala lilikuwa hapa mjini watu wengi walikuwa wanapeleka taka zao wenyewe kutupa, lakini tangu limehamishiwa huko mbali, watu wanaona uvivu na matokeo yake ndiyo haya ya kujaziwa taka nje ya nyumba zetu.
“Wanaohusika na hii biashara ya kukusanya taka mitaani tungewaona wa maana sana endapo wataamua kuwa na tija ya kufanya kazi yao na kujizatiti kunusuru huu mji kwa kukusanya taka hizi na kutuachia mazingira kuwa safi.
“Hata ukisema unafanya usafi wa mazingira ya nyumbani kwako ni bure kwani ukiamka asubuhi unakuta taka nyingine zimetupwa,” anasema mama Farida.
Anasema ha halmashauri imeamua kuendesha zoezi hilo kimaslahi zaidi badala ya kujali afya zao, kwani kila mtu anayetoa taka zake kwenye gari hilo hulazimika kulipia kiasi cha sh 1000, lakini hata hivyo haileti maana halisi katika kufanyia kile kilichokusudiwa.
Mama Farida anasema wamekosa imani kabisa na halmashauri yao na kutaka wajue kuwa kama huo mradi wa uzoaji taka ni wa mtu binafsi, kwani wabebaji taka wamekuwa wakitumia lugha mbaya kwa wateja wao ikiwa ni pamoja na kuhusika kusambaza taka hizo mitaani badala ya kuzipeleka eneo husika.
“Mwezi uliopita mimi nilitupiwa taka barazani kwangu kisa tu nilitoa taka kupeleka kwenye gari bila hela mkononi na nikawajulisha kuwa naingia ndani kutoa hela, lakini cha kushangaza dereva wa gari hilo alimwambia utingo wake azishushe taka hizo, nikiwa mlangoni kutoa hela nikashtukia taka zimetupwa barazani.
“Huu sio uungwana kabisa jamani, sasa mtu kusema naleta hela tu anatupiwa taka barazani je, akisema hana hela si ndiyo atatupiwa chumbani?
“Watuambie huu mradi kama ni wa mtu kwa maslahi binafsi tujue ili tujiandae kulifuata hilo dampo kwa miguu yetu maana kwa mtindo huu watu hawataacha kutupa taka mitaani, na huyo mkurugenzi ajipange sana la sivyo huu mji utashika namba moja kwa uchafu,” anasisitiza mama Asia.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Omary Mkombole, anasema wamejipanga kushughulikia tatizo hilo na kwamba tayari gari la kuzoa taka mjini limeshapatikana hivyo litaanza kazi muda wowote.
“Gari lililokuwa likitumika kukusanyia takataka awali halikuwa la halmashauri, tulifanya kuazima kwa mtu, lakini tayari tumeshapata gari la halmashauri na muda wowote kuanzia sasa litakuwa mtaani kukusanya takataka na kuuweka mji kuwa safi,” anafafanua Mkombole.
Anasema wananchi kutupa takataka ovyo mitaani ni tabia yao ya uchafu bila kufafanua zaidi kuhusu utaratibu wa mpango wa uzoaji wa taka uliokuwa ukifanyika awali kwa kutumia gari alilodai waliliazima.
“Wananchi wameshajiwekea utaratibu wao wa kutupa takataka ovyo mitaani, huo ni uchafuzi wa mazingira, lakini kwa sasa tumeshaweka utaratibu mzuri kudhibiti hali hiyo ili kunusuru mji wetu na kuweka mazingira katika hali ya usafi,” anasisitiza mkurugenzi huyo.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa