Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Elimu ni silaha muhimu katika kupambana na changamoto za maisha.
Hawakukosea waliosema kuwa “elimu ni ufunguo wa maisha” kwani mtu
anapokuwa na elimu ya kutosha, siyo tu atakuwa katika nafasi nzuri ya
kupata ajira, bali atapambana na mazingira yake ili kupata maisha bora.
Tangu kabla ya kuja kwa wakoloni katika karne ya
19, jamii za Kiafrika zilikuwa na mifumo mbalimbali ya kutoa elimu,
ikiwa ni pamoja na jando, unyago na kufanya stadi za kazi.
Hata hivyo walipokuja wakoloni walileta mfumo mpya wa elimu ambao umeendelea hadi leo.
Kupitia mfumo huo, watu walifundishwa kusoma,
kuandika na kuhesabu. Baada ya hapo mpangilio wa madarasa uliwekwa
kutoka elimu ya awali, shule ya msingi, sekondari hadi vyuoni.
Kupitia mfumo huu kukajengeka dhana na mpaka leo
inaendelea kuwa anayesoma mpaka madaraja ya juu ya elimu, hana budi
kuheshimika katika jamii yake.
Hii ikajenga kasumba kwa wasomi wengi kujiona bora
kuliko wanajamii wengine. Katika baadhi ya jamii usomi umekuwa na hadhi
kubwa ikikaribia ile ya watawala.
Elimu na maisha
Pamoja na kuwa elimu ni muhimu kwa ustawi wa
mwanadamu, wapo wanaoshindwa kuipata fursa hiyo kwa sababu mbalimbali
ikiwamo kufeli na hivyo kushindwa kuendelea na masomo. Hawa naomba
niwakumbushe kuwa kufeli ni sawa na ajali, hivyo hawapaswi kukata tamaa
katika maisha yao.
Mtu hapaswi kukata tamaa kwa kukosa tu elimu. Kusoma siyo kupata vyeti tu, bali ni hali ya mtu kupata ufahamu wa mazingira yake.
Kama mkulima au mfugaji atafundishwa kusoma,
kuandika na kuhesabu atayaelewa mazingira yake hivyo atapata urahisi wa
kupambana nayo.
Ieleweke kwamba, kila binadamu huzaliwa na kipaji
chake. Wapo wanaozaliwa na vipaji vya sanaa, wengine ni wabunifu wa
mashine na vifaa mbalimbali vya kurahisisha kazi.
Mathalan, kabla ya kuja kwa wakoloni na mfumo wao wa elimu,
Waafrika tayari walishakuwa na teknolojia zao. Walitengezeza majembe ya
miti na baadaye ya chuma, walitengeza mitumbwi hata kama haikuwa na
uwezo mkubwa na vifaa mbalimbali vya kurahisisha kazi.
Walipokuja Wazungu wakapuuza teknolojia hizo na
kuziita za kishenzi. Wakabadilisha na kuleta za kwao kisha wakidai
Afrika hakukuwa na maendeleo yoyote. Hiyo ilikuwa ni kudumaza akili za
Waafrika na kuwadharau.
Baada ya kutawaliwa kwa muda mrefu na Wazungu,
hata akili za Waafrika zikadumaa. Leo wengi hawaamini kama mtu anaweza
kufanikiwa kimaisha bila kupitia mfumo rasmi wa elimu. Kwamba mtu
akikosa elimu ile ya darasani ya vitabu na kalamu, basi ndiyo amekufa
maskini.
Siyo kweli, bado Waafrika tunaweza kurejea kwenye
teknolojia zetu na kuziendeleza. Inasikitisha kuona kwamba kila kitu
tunachotumia leo kimeagizwa kutoka nje ya nchi. Sisi kazi yetu ni
kutumia tu teknolojia za wenzetu siyo wao watumie zetu.
Inasikitisha zaidi kuona hata viongozi wa Serikali
wamekosa ujasiri na uelewa wa teknolojia zetu. Utashangaa kuona
wabunifu wanaounda magobore wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
Hatutaki kujua kuwa kumbe watu kama hao wangeweza
kukusanywa na kuundiwa karakana zao ili waendeleze uzalishaji kupitia
vipaji walivyonavyo.
Wapo wanaounda baiskeli, magari, matrekta na vifaa
vingine vinavyotumia vifaa halisi katika mazingira yetu, lakini
wanachoambulia ni kupewa vyeti tu na taasisi za Serikali kisha
wanasahaulika.
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia inapaswa
kuwakusanya watu kama hawa na kuwaendeleza. Mwisho tutajikuta na sisi
tunaunda vifaa vya kisayansi ambavyo tutavitumia na hata kuuza ujuzi huo
nje ya nchi.
Jambo la msingi ni kila mtu kujituma na kufanya
kazi kwa bidii ilimradi tu anayo afya na akili timamu. Kama ni kilimo,
uvuvi, ufundi mchundo na biashara basi zifanyike kwa bidii. Lazima
mafanikio yapatikane tu.
Tatizo ni kuwa vijana wengi waliokosa elimu
vijijini hawaamini kama kuishi huko ni maisha na inawezekana kuendelea
kimaisha. Wengi hukimbilia mijini wakiamini kuwa watapata maisha bora na
badala yake wamejazana mijini kufanya biashara ndogondogo.
Ni kichekesho mtu kuacha ardhi yenye rutuba kijijini kwake na kwenda mjini kuuza soksi, pipi, maji na nyembe barabarani.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment