Home » » Jaji Warioba: Wananchi wana matatizo makubwa ya ardhi

Jaji Warioba: Wananchi wana matatizo makubwa ya ardhi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Baadhi ya wabunge wakifuatilia kwa makini hotuba ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni mjini Dodoma jana.
 
Wananchi  wengi nchini wanalalamika kwamba wanayo matatizo kutokana na ugumu wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine, lakini wawekezaji wakubwa wanapata upendeleo wa kupata ardhi kirahisi.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wakati akiwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba.

Suala la Ardhi ni miongoni mwa mambo ambayo wananchi waliyatolea maoni kwa wingi kwenye Tume yake, huku wakilitolea msisitizo mkubwa wa kulipatia ufumbuzi kwenye Katiba mpya.

Jaji Warioba alisema kuna migongano isiyokwisha ya makundi mbalimbali ya wakulima, wafugaji, wananchi na mamlaka za Hifadhi za Taifa kuhusiana na suala la ardhi nchini.

Alisema kwa kuzingatia malalamiko hayo ya wananchi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imependekeza suala la kumiliki mali ikiwamo ardhi kuwa miongoni mwa Haki za Binadamu ili kuwezesha wananchi kuwa na haki ya kikatiba ya kumiliki ardhi.

Jaji Warioba alisema kuwa yamekuwapo pia malalamiko ya wananchi kuporwa ardhi yao na Serikali bila fidia au kwa kulipwa fidia kidogo, jambo ambalo alisema likiingizwa kwenye katiba litakuwa limetoa ufumbuzi wa malalamiko hayo.

Aidha, alisema tume imependekeza kwamba ikiwa Serikali itaamua kuchukua ardhi ya wananchi iwalipe fidia yenye thamani halisi ya mali au ardhi kwa wakati huo badala ya hali ilivyo hivi sasa ambapo mali ya mtu inaweza kuthaminiwa leo, lakini isilipwe kwa wakati huku tamahi ikiongezeka.

Jaji warioba alisema kuwa ili kutatua matatizo ya wakulima, wafugaji na wavuvi, Tume imependekeza malengo makubwa manne kwenye sura ya pili ya Rasimu ya Katiba.

Aliyataja kuwa ni kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kupendekeza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi na kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendelezea shughuli zao.

Mengine ni  kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na utafutaji na uendelezaji usimamiaji wa mizania ya bei za mazao na pembejeo.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa