Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MASHINDANO ya kusaka nyota wa kuboresha timu ya taifa ‘Taifa Stars’
yanatarajiwa kufikia tamati leo kwa timu mbalimbali kujitupa
viwanjani, ambako mkoani hapa, wenyeji Manyara wanawakaribisha Arusha
kwenye uwanja wa Babati.
Katika mchezo wa awali uliopigwa jijini Arusha, wenyeji waliibuka na
ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Mchezo huu unatarajiwa kushuhudiwa na waibua vipaji watano, Peter
Mhina, Zamoyoni Mogela, Elly Mzozo na Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ wakiwa
chini ya Dan Korosso.
Mbali na mchezo huo, mechi nyingine kundi A itakuwa kati ya Singida
na Dodoma, Uwanja wa Namfua na kushuhudiwa na waibua vipaji wanne,
Kanali mstaafu Idd Kipingu, Juma Mgunda, Peter Magomba na George Komba.
Kundi B, Mara watawakaribisha Mwanza kwenye Uwanja wa Karume na
kushuhudiwa na waibua vipaji watano, Salum Mayanga, Patrick Rweyemamu,
Selemani Jabir, Ahmed Simba na Mohamed Ally.
Katika kundi D, Katavi itakuwa wenyeji wa Rukwa kwenye uwanja wa
Mpanda na kushuhudiwa na waibua vipaji John Simkoko, Madaraka Bendera,
Salvatory Edward, Musa Kisoki na Sunday Manara ‘Computer’.
Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma itakuwa mwenyeji wa Tabora
na kushuhudiwa na waibua vipaji Boniface Pawassa, Edward Hiza, Yusuph
Macho na Abdallah Hussein.
Akizungumzia mashindano hayo kwa ujumla, mchezaji wa zamani ambaye
pia ni miongoni mwa waibua vipaji, Peter Mhina, alikiri kuwepo kwa
vipaji mikoani na kumpongeza Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Jamal Malinzi kwa kulitambua hilo na kuanza kulifanyia kazi.
“Malinzi kapatia sana kufanya kitu kama hiki, kwani hata sisi
tulitokea chini, kwani nakumbuka hata mimi nilikuwa nacheza timu ya
taifa wakati nikiwa kidato cha pili, hivyo basi nina imani wachezaji
watapatikana, cha muhimu ni sisi wadau kumuunga mkono Malinzi,” alisema
Mhina.
Naye Elly Mzozo, mdau na mwalimu wa soka ambaye pia ni Mwenyekiti wa
timu ya Friends Rangers, alisema anakumbana na vipaji vingi tangu
katika mechi ya kwanza ya Tanga na Kilimanjaro hadi ya Arusha na
Manyara.
Mzozo alisema anaumia kuona vipaji kama hivyo haviibuliwi huku timu ya taifa ikifanya vibaya kila kukicha.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment