Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Spika,Job Ndugai
Ndugai alitoa shutuma hizo jana dhidi ya Umbula akimuunga mkono Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, aliyemtuhumu Umbula ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Manyara, kuwa anaendesha vitendo vya kibaguzi na kukuza mgogoro huo pamoja na mauaji.
Ndugai alitoa mashambulizi hayo kwa kifupi wakati akiahirisha kikao cha Bunge hilo mchana na kueleza kuwa kilichozungumzwa amekisikia na majibu anayasikia, lakini kwa kuwa hana nafasi ya dakika saba kuchangia mjadala atazungumza kwa kifupi.
”Kinachoendelea Kiteto ni ubaguzi kama Rwanda, kama Burundi,ni ubaguzi wa kikabila tu, hakuna mapigano ya wakulima na wafugaji, ni ubaguzi hatuwezi kwenda na ubaguzi, ni aibu kubwa kwa viongozi wanaosimamia ubaguzi unaosababisha mauaji haya, this things have to stop (haya mambo yakome),” alisema.
”Jana (juzi) sijalala, wananchi wananipigia simu kuwa bunduki zinalia, watu wanauawa Tanzania, halafu anasimama kiongozi anaongea, unaongea kitu gani?” Alihoji na kuahirisha kikao.
Awali, Lema alianza kwa kumpa pole Naibu Spika kuwa kuna wakulima wawili, pikipiki 11, trekta na maduka yamechomwa moto na kwamba ni kazi ya Mkuu wa wilaya hiyo (Umbula) ambaye hivi karibuni alifanya mkutano wa wananchi na kutaka wageni na wenyeji kukaa sehemu tofauti.
”Ukiona mkuu wa wilaya anafika mahali pa kusema wageni wakae kulia na wenyeji kushoto, hiyo ni hatari kwa nchi, liangaliwe kwa umakini,” alisema Lema.
Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, alisema unapoingia kwenye jimbo lake mkono wa kushoto kilomita tisa wakati unaelekea Dodoma ni wilaya ya Kiteto na kwamba kata nzima ya Dongo watu wanaolima wilaya ya Kiteto ni wa Gairo na kwamba aliwahi kuzungumza watu wwanatengana kwa sababu ya ubaguzi.
”Kwenye Hifadhi ya Mbuga ya Embloi Murtangosi, wakulima wanasema ni hifadhi na kwamba wakulima wanafukuzwa na wafugaji kuachwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alifika na kwenda moja kwa moja kwenye kamati ya ulinzi na usalama ambao ndiyo wamesababisha majanga, walichokwambia ulikwenda kwa wananchi na kuwapa pole hukutaka kuwasikiliza,” alisema.
”Kila mara likitaka kuzungumziwa wanasema suala lipo mahakamani na watu wanaendelea kufa, naungana na Lema na Ndugai, watu wa Gairo, Kongwa na Kilindi wote wanalima pale kwa sababu ni maeneo yanayopakana,” aliongeza Shabiby.
Alisema kisingizo ni wakulima wakubwa wanachoma misitu badala yake wanastahili kupewa wadogo na kwamba naye ana shamba eneo la Kiteto.
”Twendeni tukagawe yale maeneo, kila siku hifadhi hizi tulizonazo majangili wanaingia kila siku tunashindwa kulinda gaweni kwa wakulima wajue eneo lao na wafugaji,” alisema.
Kabla ya kikao kuahirishwa, Umbula aliomba mwongozo na kusema kuwa kikao alichohutubia kilikuwa cha halmashauri kuu ya kijiji cha kijiji cha Kimana , lakini walikwenda wananchi wengi kutoka Wilaya ya Kongwa.
”Wananchi hawa ni wa jimbo lako Mheshimiwa Naibu Spika, wamezoea kutuvuruga kwa kila tunachofanya ili tusifanikiwe, napenda kutoa taarifa kuwa Godbless Lema, aelewe kuwa kikao kile ni Halmashauri ya Kijiji cha Kimana, haikutaka kujumuisha mwananchi kutoka wilaya nyingine asiendelee kuingialia na kuzungumzia masuala ambayo hayamuhusu,” alisema Umbula.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alitoa taarifa kuwa amepata taarifa za watu wawili kuuawa na kwamba alimweleza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mamgu, kuingilia kati na kwamba serikali inachukua hatua.
Akizungumza na NIPASHE nje ya viwanja vya Bunge, Umbula alisema ametoka jimboni siku tatu zilizopita na kuwa hana taarifa za vifo hivyo na uharibifu uliotokea.
Umbula alisema kwamba taarifa za watu wawili kuuawa amezisikia ndani ya ukumbi wa Bunge na taarifa alizo nazo ni mfugaji mmoja kuuawa na wakulima ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi na nyumba 42 kuchomwa moto.
Aliongeza kwamba alikwenda katika eneo hilo kuzungumza na wananchi na kupeleka chakula cha msaada.
”Mimi kama DC nilikwenda kuzungumza na Halmashauri ya kijiji cha Kimana na nikatoka nje kufanya mkutano mkuu wa kijiji ili kukubaliana mambo fulani fulani, lakini kumekuwapo na tabia kila tukifanya mkutano wenzetu wa wilaya jirani wanaleta mamluki kwa malori na matrekta kutuvuruga na ili kuepuka hilo, nikasema wasiohusika waondoke,” alisema.
Umbula alisema haoni kwamba huo ni ubaguzi kwa kuwa hawezi kuzungumza na wananchi wa wilaya nyingine kwa kuwa wahusika ni wakazi wa Wilaya ya Kiteto.
”Naibu Spika amenishutumu, lakini siyo kuanzia leo namshangaa anaelekeza shutuma kwangu wakati kuna viongozi wengi, yeye ni mkubwa, alipaswa kuniita na kuuliza na siyo kulipuka kwenye vyombo vya habari, namuachia aendelee, wananchi wenyewe watamjibu,” alisema alisema Umbula.
Alisema suala hilo linashughulikiwa kitaifa na kwamba kuna watu wanahamasisha ubaguzi ambao haupo kwani haiwezekani wilaya hiyo kugeuzwa shamba la bibi kwa watu kukopa trekta Kogwa na kwenda kulima Kiteto.
“Unapoingia eneo lazima uwe na utaratibu wa kueleweka na kukubaliana na serikali ya kijiji, nchi inatawaliwa na sheria, kanuni
na taratibu,” alisema Umbula.
Januari Ndugai alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa mgogoro huo una sura ya kikabila na kwamba viongozi wa wilaya na mkoa wanapaswa kujiuzulu nafasi zao kwa kuwa wamekuwa kichocheo cha mgogoro huo.
”DC na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa mnasubiri nini kujiuzulu, jamani hamfai kuwapo kwani hamlindi raia na mali zao na mauaji haya yanatokea bila hata mtu yeyote kukamatwa kwanini sasa nyie mpo?” Ndugai alikaririwa akihoji.
Hadi sasa zaidi ya watu 30 wanadaiwa kuuawa na kujeruhiwa baadhi yao vibaya katika eneo hilo, pamoja na mali mbalimbali kuharibiwa vibaya kwa kuchomwa moto tangu mgogoro huo ulioanza miaka minane iliyopita.
Mwaka jana yaliibuka mapigano yaliyosababisha vifo vya watu takribani 14, hali iliyomlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutembelea eneo la mapigano.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment