Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI zaidi ya 3,000 wa Kijiji cha Hedet, Wilaya ya Hanang mkoani
Manyara, kwa zaidi ya miaka miwili sasa hawana huduma ya maji safi na
salama kutokana na baadhi yao kuvamia na kuondoa stesheni kuu za
kusambazia maji zilizokuwepo kwenye njia kuu katika vijiji vya Mara na
Getaghul.
Malalamiko hayo yalitolewa na wananchi hao kwa Mbunge wa Hanang,
ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji na Uwezeshaji),
Dk. Mary Nagu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha
Hedet.
Walifafanua kuwa pamoja na kuchangia sh. 6,000 kwa kila kaya, lakini
wameendelea kunywa maji yasiyo salama huku wakichangia huduma hiyo
pamoja na mifugo.
Kwa sasa wananchi hao wanasema wapo tayari kuandamana kuishinikiza serikali kuwapatia maji.
Awali katika taarifa ya Kijiji cha Hedet, iliyosomwa na Ofisa
Mtendaji, Bahati Tarimo, walimweleza Waziri Nagu kuwa kijiji hicho
hakina huduma ya maji safi na salama tangu Juni 2012, kutokana na
wananchi kung’oa stesheni kuu za kusambazia maji katika njia kuu ya
kusambazia maji hayo.
Waziri Nagu akijibu malalamiko hayo, alimuagiza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kuzungumza na wazee wa vijiji
vinavyogombea maji.
Pia aliwataka wahakikishe wanaweka utaratibu wa kuchimba visima
virefu katika vijiji vya Mara na Getaghul ili kuondoa ugomvi wa maji na
kusababisha mabomba kukatwa.
Hata hivyo, katika ziara hiyo ya siku tano wilayani Hanang, Waziri
Nagu awali alitembelea na kukagua zahanati inayojengwa, tenki la maji
pamoja na sehemu ya kunyweshea mifugo ya vijiji vya Gidagharubu pamoja
na kukagua ujenzi wa nyumba za watumishi wa Idara ya Afya zinazojengwa
kwa ufadhili wa taasisi ya Mkapa Foundation
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment