Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Vitendo viwili vichafu “vinavyofichwa” na watawala duniani ni
biashara ya dawa za kulevya na unyanyasaji wa watoto. Ingawa ni vya aibu
na ufedhuli vina faida sana kwa wahusika. Dawa za kulevya ni biashara
inayotajirisha haraka kuliko zote.
Ripoti iliyotolewa na Idara ya Kuzuia Uhalifu na
Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa (UNIDOP) mwaka 2011, inasisitiza
asilimia 20 ya kipato cha dunia hutokana na biashara hii ya ki-Ibilis.
Ndiyo maana mtu yeyote anapopambana na ujambazi huu lazima atauawa. Haya
yanaonekana Mexico - kilele cha ujambazi wa dawa za kulevya. Video za
mauaji – wakiwepo wanawake na vigori- wakikatwa katwa kwa mapanga, visu
na mashoka zimeselelea mitandaoni.
Habari za Watanzania waliokamatwa wakibeba unga au heroini ughaibuni sasa zimekuwa nongwa.
Unyanyasaji wa watoto hauna faida ya kiuchumi ila
ni “jaha” kwa wahusika. Hali kadhalika ni rahisi kuwatumia watoto kubeba
silaha, mizigo, kuwalawiti, nk.
Wiki hizi mbili zilizopita Uingereza imeshuhudia
sokomoko la wakuu wa nchi walivyofanya kila njia kuzuia habari za ngono
na watoto kutofichuliwa.
Madai yalifanywa na mmoja wa vizito ndani ya
serikali ya chama cha Conservative kati ya 1979 na 1990. Inadaiwa
mafaili yaliyotayarishwa na marehemu Geoffrey Dickens mwaka 1983
yaliharibiwa baada ya kufikishwa polisi. Uongozi wa sasa wa Waziri Mkuu,
David Cameroon umethibitisha kuwepo kwa mafaili 746,000, ofisi za
Wizara ya Mambo ya Ndani kati ya 1979 na 1999. Miongoni ya hayo 114
yaliyoharibiwa, 13 yanahusu uchunguzi wa unyanyasaji wa watoto. Neno
linalosikika ni “paedophilia”- yaani tabia ya mtu mzima kuhusudu mapenzi
au ngono na watoto.
Bado madai yanaendelea kujadiliwa serikalini. Dai
muhimu lasema viongozi wa ngazi za juu, wakiwapo wanadini na familia ya
malkia walihusika. Aliyekuwa madarakani wakati huo ambaye sasa hivi ni
mstahiwa mwenye hadhi ya “Lord” ...anadaiwa alimbaka mwanafunzi wa miaka
19 mwaka 1967.
Kidesturi wadhifa wa “Lord” unatokana na umwinyi
Uingereza na familia ya wafalme. Leo mtu yeyote aliyeifanyia mazito
jamii anaweza kuteuliwa kuwa Lodi. Wanawake huitwa Baroness. Mfano ni
Mjamaika, Baroness Doreen Lawrence ambaye mwanaye, Stephen, aliuliwa na
wabaguzi wa Kizungu, London, mwaka 1993. Baroness Lawrence amepigania
haki ya mwanaye kirefu hadi kuwapeleka baadhi ya wahusika jela.
Moja ya manufaa ya “Malodi” (neno lililoingia
ndani ya msamiati wa Kiswanglish) huruhusiwa kuingia kikao maalumu cha
wabunge. Kikao kina nguvu za kupitisha miswada na sheria za serikali.
Tuendelee.
Dai la pili la kashfa hii inayoitetemesha
Uingereza- linasema uongozi wa enzi za marehemu Margaret Thatcher
ulijaribu vilevile kubatilisha sheria za kuruhusu watoto chini ya umri
wa miaka 16 kufanya ngono. Wiki jana kamati ya uchunguzi
ilitahadharishwa kutoficha baadhi ya madai ikiwapo jina la askofu
maarufu aliyelawiti watoto.
Haya mambo yapo kila mahaliuakini hayasemwi. Kwetu
Tanzania- miaka mingi- tabia ya watu wazima au wenye nafasi kubwa
kulala na watoto imeenea. Chawa ameanza kuonekana karibuni kutokana na
mjadala kuhusu ushoga.
Miaka mitatu sasa Serikali za Kizungu –zikiongozwa na Wamarekani
zimetutaka Waafrika kulegeza sheria za mapenzi ya jinsia moja. Kinyume
na namna uhusiano huu unavyokuwa nchi zilizoendelea. Ushoga, kwetu si
utamaduni na wale wanaofanya huwa wamelazimika.
Mtafiti na mchunguzi aliyetuma makala ya kurasa tatu ndani ya moja ya mitandao jamii inayosomwa na Waswahili. Anadai:
“Sidhani Marekani inatutaka tukubali ushoga. Ni
kunyanyasa na kuonea ndiyo inataka tuache maana...hawa tunawatengeneza
wenyewe kwa kulawiti vitoto... watu wenye mahitaji tunatumia ngono kama
chombo.”
Nakubaliana na mwandishi. Zamani nikisoma shule za
kulala za sekondari ilikuwa kawaida baadhi ya wavulana kufanywa
wanawake kwa nguvu na vijana wakubwa zaidi. Wapo waliopigana na
walioshindwa. Walioshindwa waligeuka mashoga. Mmoja niliyesoma naye
Mzumbe mathalan ( vitendo viliitwa “umbuzi”), alikuja kuwa shoga
maarufu.
Si shuleni tu. Mtafiti anaendelea kusema “Malezi
ya nyumbani –kulaza watoto wadogo wa kiume na wakubwa wanaonea wadogo
kisha wanazoea – kwa asilimia 80. Mlinzi, dereva wa watoto, mtoto wa
kazi za nyumbani analawiti wanao wewe mwajiri huju. Dereva humfungi
maisha unamfukuza kazi; unapokuja kufahamu mwanao keshazoea. Humsaki
aliyemfanya hivyo. Hausigeli anasaga vitoto au wadogo zake.”
Ni mambo yanayotokea majumbani, kisirisiri, tunayafahamu na hatuyapingi.
Mwandishi anaelezea utafiti aliofanya Dar es
Salaam kuhusu ulawiti. Anadai siku hizi ili kupata ajira, kinachotakiwa
si fedha bali ngono: “ Kwa changudoa kipato ni kikubwa zaidi asipotumia
kondom au akikubali tigo. Wafanyao haya ni waume za watu, waheshimiwa,
watu wa dini, wenye hela, kampuni, hoteli – wenye vipato. Wasichana
wanahadaiwa, hatimaye wanaharibika.”
Mbali na ulawiti unaoendelea mitaani, shuleni na
katika taasisi za kidini (mathalan madrassa) mtafiti anagusia tatizo la
homoni. Homoni au “hormones” kwa Kiingereza ni viini vinavyoendesha
mizunguko na tabia za maumbile. Watu wanaogeuka jinsia zao kutokana na
kulawitiwa wakiwa wadogo au ujanani kihomoni ni wengi Tanzania anadai
mchunguzi.
“Zamani wazee wa mila walikuwa wakiwavunja lakini
siku hizi tunawaficha hatuna mila za kikabila tunazozifuata na
kuwasaidia. Hospitali ni gharama. Aibu. Mbona wapo wanaume wenye viuongo
vya kike na kiume na wameoa?”
Madai mazito.
Suluhisho nini?
Vyombo vyetu vya habari bado havithubutu kujadili.
Bado tunajificha katika shuka za mila na desturi. Wanaoumia ni watoto
na watu wazima walioharibiwa vijijini na mijini
Misaada ijayo kupitia taasisi na vyama mafichoni haiwafikii, inaliwa na wachache bila kuwapa huduma ya hospitali na ajira.
Halafu vipi mtu aliyelawiti au kuharibu watoto
anapokamatwa mbona ndugu zake humtolea dhamana na kumnyanyasa mtoto au
kijana aliyebakwa?
Kwa nini tunaruhusu hawa watesaji kutembea njiani
huku tukiwanyanyasa walioharibiwa na kugeuzwa mashoga? Viongozi wetu
hasa wabunge wanapashwa kupitisha sheria kali kuwatia nguvuni
wanaoharibu watoto. Lakini je, Serikali yetu iko tayari kufukua handaki
na shimo hili la kiza?
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment