Home » » WAFANYAKAZI TANESCO KUJADILI HATIMA YAO

WAFANYAKAZI TANESCO KUJADILI HATIMA YAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga
Wakati kuna taarifa za mabadiliko makubwa ya kuligawa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika kampuni tatu, wafanyakazi wa shirika hilo wamesema wako tayari na wanajiandaa kujadili hatima yao.
 Shirika hilo litagawanywa katika kampuni tatu za uzalishaji, usafirishaji na ugawaji kwa kinachoelezwa kuwa ni kuboresha utendaji.

Gazeti la kila siku la serikali toleo la Juni 23, lilikariri habari kutoka ndani ya Baraza la Mawaziri zikieleza kuwa chini ya mabadiliko hayo utekelezaji utaanza mwaka huu na mpango wa awali unahitaji kiasi cha Sh. bilioni 11.4 kati ya mwaka 2012-2017.

Imeeleza kuwa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2014/15 unatarajiwa kutumia kiasi cha Sh. bilioni 565.71, ikiwa ni fedha za nguvu kazi, elimu na kulipa malimbikizo mbalimbali.

Imeeleza kuwa uzalishaji wa umeme unatarajiwa kuongezeka kutoka megawati 1,583 hadi 10,000 ifikapo mwaka 2015.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa utekelezaji wa kugawa shirika hilo unatarajiwa kufanyika kati ya mwaka huu na mwaka 2025, ikiwa katika vipindi vya Julai 2014-2015 kipindi cha muda mfupi, 2015-2018 kipindi cha kati na kipindi kirefu cha mwaka 2021-25.

Katibu wa Tawi la Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (Tuico), Ernest Mwakikoti alisema Mei mwaka huu, Wizara ya Nishati na Madini  iliitaarifu tawi la wafanyakazi kuhusu mchakato huo na kwamba hadi kufikia Desemba mwaka huu, kitengo cha uzalishaji kitakuwa kimeshagawanywa.

Alisema wameitisha kikao cha viongozi wa kanda mbalimbali wanaounda kamati ya majadiliano kitakachofanyika Julai 15 na 17, mwaka huu, mkoani Tanga ili kuwapa taarifa viongozi ili wawafahamishe wafanyakazi juu ya mchakato huo.

“Tukiwafahamisha utaratibu wa wizara tunatarajia kupata maoni yao juu ya suala hilo,” alisema Mwakikoti ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya majadiliano itakayokutana mkoani Tanga.

Alisema kwa mujibu wa maelezo ya Wizara, kampuni ya kwanza ya uzalishaji itakuwa imekamilika kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kampuni ya usafirishaji itagawanywa hadi kufikia 2016 na usambazaji mwaka 2017-19).

 Alisema watakapokutana na viongozi wa matawi watajadili kwa kiana ikiwamo suala la wafanyakazi ingawa kauli ya wizara hakutakuwa na kupunguza wafanyakazi.

Alisema wafanyakazi wa Tanesco wapo wanaostaafu na kwa mwaka huu watakuwa 100 na kwamba kama kutakuwa na kupunguzwa wamejiandaa katika mkataba wa hali bora kazini ambao unaainisha mafao ya mfanyakazi.

“Sisi hatuna hisa Tanesco, tumelipokea hili kama baba anavyoweza kufanya maamuzi ndani ya familia yake, tutapokea kama lilivyo, tunaamini mgawanyo huu utaleta mabadiliko makubwa.

Hata hivyo, Tanesco walipoulizwa juu ya mabadiliko hayo, Msemaji wake, Adrian Severin, alisema utaratibu wote upo wizarani na wao ni watekelezaji wa maagizo yatakayotolewa.

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga alisema hadi sasa hakuna uamuzi wa jumla uliofikiwa wa kuligawa shirika hilo bali ni mapendekezo yaliyopelekwa kwa wataalamu mbalimbali wajadiliane na kuwasilisha serikalini.

Alisema baada ya mapendekezo hayo kupokelewa serikali itaangalia cha kufanya kwa kuangalia mambo makuu matatu.

“Kabla ya kuanza kutekeleza mapendekezo husika tutaangalia mahitaji ya Taifa, Dira ya taifa ya mwaka 2025 na mpango mkakati wa Taifa wa miaka mitano mitano, baadaye tutaamua lini na ifanyike kwenye mgawanyo huo,” alisema.

Kwa mujibu wa Kitwanga, timu mbalimbali zitakusanya mapendekezo ya wadau na hadi sasa hakuna uamuzi wa jumla wa serikali  na kwamba yote yanafanyika katika kuboresha shirika hilo.

Alisema baada ya kukusanya maoni ya wadau na kuyachambua ndipo serikali itaendelea na mchakato wake.

Naibu Waziri huyo alisema hakuna mfanyakazi atakayepunguzwa kwa kuwa kutakuwa na mahitaji ya wafanyakazi wenye uwezo mkubwa wa kulitumikia shirika katika kufikia mafanikio tarajiwa.

Alisema kwa sasa shirika linahudumia asilimia 36 ya Watanzania na linataka kufikia asilimia 100 hivyo inaweza kufikiwa kwa kuwa na wafanyakazi wa kutosha.

“Wafanyakazi wasitishwe na mchakato huu, shirika likigawanywa litahitaji idadi kubwa ya wafanyakazi wenye uwezo ili kuifikia asilimia 64 ya Watanzania wanaohitaji huduma ya umeme,” alisema Kitwanga.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa