Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI wa Kata ya Gisambalang’, Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara
bado wanaendelea kugubikwa na wimbi la simanzi na majonzi kutokana na
matukio ya mauaji mfululizo yanayotokea katika kata hiyo.
Katika Kitongoji cha Langasesi, Kijiji cha Warang’, usiku wa kuamkia
Julai 28, mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Daniel (32),
ameuawa kwa kupigwa na jirani yake, Phiri Mampo (33), kwa tuhuma za
kutembea na mke wake.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa kata hiyo, Masalla Bajuta, alisema
kwa mujibu wa maelezo ya mtuhumiwa baada ya kumhoji, siku ya tukio
Daniel alikuwa amekwenda nyumbani kwa mtuhumiwa ambako alimkuta amelala
na kumdai mke wake chakula.
Alisema wakati mwanamke huyo akiandaa chakula, mume wake aliamka na
kuwakuta wametoka nje ya nyumba, ndipo alipowafuata na kuanza kumvamia
Daniel na kumpigiza ukutani ambapo aliangukia kichwa na kufariki papo
hapo.
Diwani huyo alieleza kwamba, baada ya Mampo kuona jirani yake
ameshindwa kuamka, alimuangalia na kugundua amefariki, ndipo
alimuamrisha mke wake amsaidie kumbeba na kumtupa takribani mita 600
kutoka nyumbani kwao huku wakiwa wamemuwekea ulinzi kama kuna watu
watamuona.
Alibainisha kuwa maiti ilishinda eneo hilo hadi Julai 29 majira ya
saa 12 jioni, ambapo watoto waliotoka kuchunga waliiona na kukimbia
nyumbani kwao kutoa taarifa kwa wazazi wao ambao ni jirani na kwa
mtuhumiwa.
Diwani huyo aliongeza kuwa jirani huyo aliyejitambulisha kwa jina la
Gitimai aliikuta maiti na kukimbia kwa mwenyekiti wa kitongoji na
wakati wanaelekea eneo hilo, mtuhumiwa alishagundua kuwa imeonekana
hivyo alichukua jukumu la kuihamisha eneo jingine mbali na mahali hapo.
Watu walipofika eneo la awali, hawakukuta maiti zaidi ya damu.
Alisema kuiwa waliamua kupiga yowe na wananachi zaidi walijaa na
kabla hawajaanza msako, walikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa na kumhoji
ila alikataa, lakini wakati huo mke wake alikuwa akilia na kuamua
kueleza kilichotokea, ndipo mtuhumiwa alikamatwa na kwenda kuonyesha
alipouficha mwili wa marehemu.
Wananchi wa kata hiyo, wamelaani vikali kitendo hicho na wamesema
kuwa wameamua kufanya maombi kila mmoja kwa imani yake kumuomba Mungu
awaondolee matukio hayo, kwani siku hiyo hiyo mtoto aliyekadiriwa kuwa
na miaka mitano alifariki dunia kwa kugongwa na pikipiki na dereva
kukimbilia wilaya ya jirani ya Kondoa.
Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Deusdedit Nsimeki, alithibitisha
tukio hilo na kusema kuwa marehemu, mtuhumiwa pamoja mwanamke
aliyesababisha tukio hilo, wote walikuwa wamelewa.
Kamanda Nsimeki, alisema watuhumiwa wamekamatwa na wako ndani kwa
mahojiano na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment