Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU saba wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani Manyara,
akiwemo daktari bandia na wengine katika mtandao wa wizi wa magari
uliyotokea jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti.
Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Deusdedit Nsimeki, alisema wamemtia
mbaroni Godlone Sozigwa (27), mkazi wa Dar es Salaam ambaye
alijifanya daktari katika hospitali ya mkoa akiwa amepeleka maombi ya
kufanya kazi kwa muda.
Nsimeki, alieleza kwamba Sozigwa alikuwa na vyeti mbalimbali vya
kughushi ambavyo vilionyesha amehitimu elimu ya udaktari chuo cha
Muhimbili huku akiwa na mavazi rasmi ya udaktari.
Alibainisha kwamba mtuhumiwa alikamatwa kupitia wasiri wa jeshi hilo
pamoja na kushindwa kujibu maswali kadhaa ya kitaaluma wakati akihojiwa
baada ya kupokelewa maombi yake.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Sozigwa alikiri kughushi
vyeti na kuomba kazi kutokana na hali ngumu ya maisha inayomkabili,
huku akidai alisomea taaluma hiyo katika kampuni moja ya Kichina ambayo
alikuwa akifanya kazi jijini Dar es Salaam.
Alisema alisomea taaluma hiyo kwa miaka minne na aliona anao uwezo wa
kuhudumia wagonjwa kama madaktari wengine, hivyo akaona ili kujikimu
kimaisha atume maombi katika hospitali hiyo ambayo alidai aliambiwa kuna
uhaba wa madaktari.
“Nikweli hivi vyeti nimefoji, lakini mimi na wenzangu tulisomea
udaktari kwa muda wa miaka minne katika kampuni moja ya kichina ambako
tulikuwa tukifanya kazi na kilichonifanya kufanya hivyo ni ugumu wa
maisha unaonikabili,” alieleza mtuhumiwa huyo.
Aidha, Kamanda Nsimeki, alisema watuhumiwa watano waliohusika kwenye
wizi wa gari aina ya Canter Toyota lenye namba T 233 CMR eneo la
Mbagala kwa kuvushwa kwenye uzio, wamerudishwa jijini Dar es Salaam
baada ya uchunguzi kukamilika.
Aliwataja kuwa ni Said Salum (36), ambaye ndiye alikutwa na gari hilo
na Albert Philipo (46), wakazi wa Negamsi mjini Babati, Hamad Ally
(32), mkazi wa Maisaka mjini Babati, Hamisi Juma (48), na Hashim Hassan
(49), wakazi wa mkoani Arusha.
Kamanda alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Rajab Marobo (42), ambaye
anahusishwa na wizi wa gari aina ya Spacio yenye namba T 498 CCC
iliyoibiwa Tabata Dar es Salaam ikiwa kwenye maegesho, ambako imedaiwa
dereva wa gari hilo alipanga njama na mlinzi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment