Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Wilaya
ya Babati vijijini mkoani Manyara kwa kipindi cha mwezi Juni 2013 hadi
Juni 2014 imekusanya jumla ya sh.1,758,784,299 kutokana na mapato yake
ya ndani ambayo ni sawa na asilimia 94 ya makisio ya mwaka ambayo
yalikuwa sh. 1,867,801,000.
Hayo yalisemwa juzi na
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Bw. Dominic
Kweka, wakati akisoma taarifa ya Halmashauri, kwenye kikao cha Baraza la
Madiwani cha kufunga mwaka wa fedha kilichohudhuriwa na wakuu wa idara
pamoja na wananchi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Akisoma taarifa hiyo ya
halmashauri yao kufanya vizuri katika makusanyo ya ndani, Bw. Kweka
alisema, ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani umewawezesha kupata hati
safi na kutaka juhudi hizo ziendelee ili kuiweka halmashauri pazuri
kimaendeleo.
Naye kwa upande
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw. Nicodemas Tarmo akifungua kikao
hicho aliwataka watumishi kuzingatia kanuni za utendajikazi kwa kufanya
kazi kwa uadilifu na kuepuka tabia za utoro na ulevi saa za kazi.
Bw.Tarmo alisema,
"watoro na walevi kazini wasilelewe kwa kutafuta visingizio bali
wachukuliwe hatua za kinidhamu na siyo kuwahamisha na kuwapeleka maeneo
mengine na kwenda kuambukiza matatizo kwa wengine, hasa walevi ni bora
tubaki na wanywaji lakini siyo walevi."
Pia Bw. Tarmo
aliwahimiza madiwani katika kata zao kufanya kazi ya ziada ya
kuwashawishi wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ili
kuboresha huduma ya afya vijijini kwani inaonesha kwamba ujumbe huo bado
haujawafikia wananchi walio wengi.
Kwa upande wa migogoro
ya ardhi iliyokithiri katika halmashauri hiyo, Bw Tarmo aliwataka
madiwani waelimishe jamii kupitia mikutano itakayokemea vyanzo vya
migogoro na kuzuia uuzaji holela wa ardhi unaofanyika mitaani bila
kushirikishwa halmashauri za vijiji kwani ndiyo wenye dhamana ya ardhi
kijijini.
Aidha katika kikao
hicho, mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na ukosefu wa chakula cha mchana
kwa shule za msingi, ambapo Diwani wa kata ya Bashnet, Bw. Laurent Tara
aliposema kwamba inashangaza kuona wito huo wa kuchangia chakula cha
mchana kwa watoto wa shule za msingi unakuwa mgumu ilhali wananchi
haohao wanakubali kuchangia chakula kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Akichangia hoja hiyo
Bw. Tara alisema, "kwa nini wazazi wanashindwa kuwahurumia hawa watoto
wadogo wa shule za msingi kwa kuwachangia chakula cha mchana na badala
yake wanakubali kuwachangia wale wakubwa walioko sekondari, mbona huu ni
ukatili tuchukue hatua za kumaliza tatizo hili.”
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment