Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katika utawala wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa na uchumi
huria, kuendeleza mfumo uleule wa kizamani katika medani ya siasa,
mathalan, dhana ya “chama tawala”; “chama kushika hatamu za uongozi”;
“chama kimoja”; “zidumu fikra za mwenyekiti”, kwa moyo wa dhati kabisa,
lazima niseme kwamba, kwa mtindo huo, Watanzania tutajikaanga kwa mafuta
yetu wenyewe.
Mabadiliko au mageuzi ya kiuchumi tuliyoyatarajia
hayatakuwepo asilani . Nchi za wenzetu duniani, na hata za majirani
zetu, zitasonga mbele kiuchumi, tena kwa kasi, lakini sisi tutabakia
hapa tulipo, na pengine tukarudi nyuma zaidi kimaendeleo.
Kwa sababu, sisi tutakaposinzia, tutawapa mwanya
wenzetu wa nje waje zaidi kuwekeza nchini. Wachote zaidi
kilichopatikana, na kukipeleka kwao, wakituacha na umaskini wetu.
Tumekiona hicho kikifanyika katika sekta ya madini
na rasilimali nyingine za nchi, ambazo Watanzania wenyewe hawakuwa na
ubavu wa kuwekeza vilivyo.
Ukweli ni kwamba Watanzania tutaendelea
kujikongoja kwa mwendo wa Konokono, tukiomba Mungu tusipishane na gari
yanayoendeshwa na wawekezaji kutoka nje wenye mitaji mikubwa’.
Watanzania tutabakia tumenasa, na hata ikibidi kuzama zaidi katika lindi la ufukara na umaskini .
Watu hawatakuwa na uwezo wa kuwekeza na kuendesha
miradi mikubwa ya kiuchumi yenye uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa
haraka (BRN), kama wengi walivyotarajia.
Kwa nini ? Kwa sababu tutakuwa tumekubali kuruhusu
ushindani katika uchumi, yaani nguvu za soko na sekta binafsi ziongoze
uchumi na biashara.
Lakini, bado tutakuwa wagumu au tumeshikwa na
kigugumizi katika kuruhusu ushindani wa kweli katika medani ya siasa kwa
kuruhusu au kukubali kuwa na Katiba mpya itakayoruhusu na kufungua
milango ya ushindani wa kisiasa, na Katiba hiyo mpya kuwa mhimili wa
kweli wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kwa kutengeneza uwanja
ulio sawa wa ushindani wa kisiasa, miongoni mwa vyama vya siasa nchini,
bila kuruhusu ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Wenzetu wamepiga hatua kubwa kiuchumi kwa sababu
ya ubora na umakini wa katiba zao. Katiba zao zimejenga ushindani wa
kisiasa uliokidhi mahitaji ya ushindani wa kiuchumi .
Kwa kuwa tumekubali ushindani wa kiuchumi, hatuna
budi kukubali ushindani wa kweli na wa haki kisiasa. Vitu hivyo viwili
daima huenda pamoja, vikiachana lazima patatokea mtafaruku kimaendeleo.
Ziko wapi tena nguvu za umma katika vyama vya
siasa, wakati mashirika yao ya umma yaliuawa na wajanja wachache na wao
wakaachwa yatima ?
Ziko wapi tena zama za nguvu ya umma, kwa kutoa ahadi za nafasi
nyingi zaidi za ajira, na hali bora zaidi ya maisha, wakati viwanda vyao
vilipukutika na kubakia maghofu na nchi kugeuzwa dampo la bidhaa duni
kutoka nje?
Wakati migodi yote muhimu ikimilikishwa kwa wageni
(kampuni za kimataifa), na wao wakibakia na vumbi lisilo na utajiri wa
uhakika?
Katika mazingira kama hayo ya uchumi shindani,
bila ya kuruhusu siasa shindani itakayoongoza na kulindwa na Katiba mpya
na bora, iliyobeba maudhui hayo ya mageuzi ya kiuchumi, basi tujue kwa
hakika kwamba Watanzania tutajikaanga kwa mafuta yetu wenyewe.
Hakuna cha maana kitakachofanyika kiuchumi katika
dunia hii ya utandawazi. Utegemezi wa kiuchumi na kiteknolojia utazidi
kuongezeka kwa kukosa ubunifu wa kifikra na mawazo mbadala.
Tony Adams ni mchambuzi wa masuala ya uchumi anapatikana kupitia barua pepe: majaliwa.adamms@gmail.com.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment