Home » » SEKONDARI YA NAINOKANOKA YALIA UHABA WALIMU WA SAYANSI

SEKONDARI YA NAINOKANOKA YALIA UHABA WALIMU WA SAYANSI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
SHULE ya Sekondari ya Nainokanoka wilayani hapa Mkoa wa Arusha inakabiliwa na ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi licha ya kuwa na mchepuo huo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Blandina Francis, alipokuwa akitoa shukurani kwa viongozi wa baraza la wafugaji waliotembelea kukagua mradi wa maabara na nyumba za walimu
uliogharamiwa na baraza hilo kwa zaidi ya sh milioni 223.
Mwalimu Blandina, alisema licha ya shule hiyo kupata maabara ya kisasa (multipurpose), kwa ajili ya masomo hayo, lakini bado ina changamoto ya kutokuwa na walimu wa kufundisha somo la fizikia.
Alisema shule hiyo ina uhaba wa walimu hao, kwani waliopo ni wawili tu na wanafundisha kemia na bailojia, lakini fizikia hakuna kabisa mwalimu hali inayoleta changamoto kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi.
Mkuu huyo wa shule, alisema wana kidato cha tatu na mwakani watakuwa na kidato cha nne kwa mara ya kwanza, lakini changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa walimu wa masomo hayo pamoja na hali ya mazingira, kwani eneo hilo ni la baridi sana na kusababisha baadhi ya wanafunzi kupata magonjwa ya baridi yabisi mara kwa mara.
Pia, aliishukuru NCAA na Baraza la Wafugaji kwa kuwezesha ujenzi wa maabara hiyo ya kisasa iliyogharimu sh 149,333,814.32 pamoja na nyumba za walimu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro, Metui Ole Shaduo, alisema baraza hilo litaendelea kusaidia jamii ya wafugaji wanaoishi ndani ya Bonde la Hifadhi ya Ngorongoro, hususan katika sekta ya elimu ili kuwa na wataalam wengi wa jamii hiyo katika masuala ya sayansi na kutoa rai kwa wazazi kuwapeleka watoto shuleni wapate mwanga kusaidia familia zao.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa