Home » » SERIKALI YAOMBWA KUSAIDIA CHAKULA NGORONGORO

SERIKALI YAOMBWA KUSAIDIA CHAKULA NGORONGORO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SERIKALI imeombwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha inasaidia wananchi waishio katika Tarafa ya Ngorongoro ambao hivi sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula na kuchangia mahudhurio duni ya wanafunzi shuleni.
Ombi hilo, limetolewa mwishoni mwa wiki na Diwani wa Kata ya Nainokanoka, Edward Maura, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea hali ya elimu wilayani Ngorongoro hivi sasa na jitihada zinazofanywa na baraza la wafugaji kupunguza changamoto hizo.
Maura, alisema hali imekuwa mbaya sana baada ya Shirika la Chakula duniani (WFP), kujitoa kusaidia misaada ya chakula katika shule za Msingi, hivyo kusababisha wanafunzi wengi jamii za kifugaji hivi sasa kutohudhuria masomo kutokana na hali ya njaa iliyopo.
“Kipindi kirefu WFP ilikuwa ikitoa huduma ya chakula katika shule zote za msingi ndani ya Tarafa ya Ngorongoro na kuvutia watoto wengi kuhudhuria masomo darasani, lakini toka limesitisha huduma hiyo hali sasa ni mbaya sana si tu mashuleni bali hata majumbani”, alisema Maura.
Alifafanua kuwa, wao kama Baraza la Wafugaji Ngorongoro kutokana na msaada huo uliokuwa ukitolewa na WFP, waliamua fedha zote za ruzuku zinazotolewa na Mamlaka ya Ngorongoro kwa Baraza hilo, kuzielekeza katika kusaidia miundombinu ya elimu na ufadhili wa ada kwa wanafunzi
wanaotoka katika familia duni.
Alisema jitihada hizo zimewezesha kusaidia miundombinu ya elimu katika tarafa hiyo, hususani upande wa shule za Sekondari, ambako tarafa hiyo ina shule mbili za Nainokanoka na Embarway ambayo hivi sasa ina kidato cha tano.
Alitoa wito kwa serikali kuchukulia suala la uhaba wa chakula katika tarafa hiyo kama ni janga na kuchukua hatua za dharura kunusuru hali hiyo kabla ya kuwa mbaya zaidi na kusababisha vifo kwa wafugaji waishio ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro ambao wamezuiwa kulima kwa lengo la kujipatia chakula.
 Chanzo Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa