Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo amewataka askari wa Usalama Barabara (trafiki), kuacha kuwa na huruma nyingi pale wanapokamata magari yenye matatizo.
Badala yake, amewataka wafanye kazi kwa bidii ili kupunguza ajali za barabarani.
Mbwilo alisema hayo jijini hapa jana alipokuwa akifunga Wiki ya Nenda kwa Usalama iliyokuwa ikifanyika Kitaifa Arusha, iliyopewa kaulimbiu isemayo “Maamuzi yako Barabarani ni Hatima yetu- Fikiri Kwanza”.
Alisema ni aibu kwa trafiki kuwa na moyo wa huruma kila wakati, yaani kupokea rushwa, bali kila mtu anayefanya makosa achukuliwe hatua zinazostahili.
Alitoa rai kama mtu anaweza kuhonga, basi ahonge Sh milioni 1 kwa makosa ya barabarani, badala ya askari hao kupokea Sh 1,000 au wakati mwingine Sh 500 kama rushwa barabarani.
Alisema si busara kwa viongozi wa Serikali, kuwataka madereva wao kuendesha magari bila ya kupumzika.
Chanzo;Habari Leo
Alitoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri, kuacha tabia ya kutowapa mikataba ya ajira wafanyakazi wao ili waweze kuwa na uhakika wa kuendesha vyombo hivyo na majukumu yao kifamilia.
“Ni aibu kwa trafiki kupokea buku au Sh 500 fanyeni kazi kama mtu anataka kukuhonga ni vyema atoe hela nyingi lakini pia nyie wamiliki wa vyombo vya usafiri toeni mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wenu pia nyie trafiki hakikisheni magari yanayokwenda safari ndefu yanakuwa na madereva wawili ili kupunguza ajali”, alisema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Usalama Barabarani ambaye pia ni Kamanda wa Trafiki Nchini, Mohammed Mpinga alisema kwa miezi nane iliyopita, idadi ya ajali imekuwa ikidhibitiwa.
Hata hivyo, alisema madhara ya ajali hizo, yameongezeka katika kipindi cha miezi mitatu. Alisema Januari mwaka huu, kulitokea ajali 1,864, zilizosababisha vifo 320 na mwezi Agosti 2014 kulitokea ajali 1,146 zilizosababisha vifo 390.
Ajali zilizotokea katika kipindi cha miezi nane zilikuwa 10,586, wakati mwaka jana ajali 15,682 zilitokea kati ya Januari na Agosti. Alisema madhara, vifo na majeruhi yamepungua huku vifo vikiwa ni watu 40 na majeruhi 3,603.
Ajali za bodaboda zilikuwa 4,467 kati ya Januari na Agosti mwaka 2013 na waliofariki ni 704 na majeruhi 4,312. Kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu ajali za pikipiki zilikuwa 3,998, zilizosababisha vifo 608 na majeruhi 2,883.
0 comments:
Post a Comment