Home » » ZACHARIA: NILIOMBA UTUMISHI KWA WANANCHI, SIYO UBOSI

ZACHARIA: NILIOMBA UTUMISHI KWA WANANCHI, SIYO UBOSI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Mirerani. Kata ya Endiamtu iliyopo Mkoa wa Manyara, ndiyo inayoongoza kwa kuwa na maendeleo wilayani Simanjiro. Kata hiyo yenye idadi ya watu 29,000 ina shule saba za msingi, ambapo tatu ni za Serikali na nne za watu binafsi, ina shule moja ya sekondari na ina kituo kimoja cha afya na zahanati moja ya taasisi ya kidini.
Diwani wa kata hiyo, Lucas Chimbason Zacharia (38) ambaye pia ni Katibu wa Uchumi wa CCM, Manyara, pamoja na mambo mengine anaeleza changamoto anazokabiliana nazo.
Swali: Ni lini ulikuwa diwani kwa mara ya kwanza na nini kilikusuma ugombee nafasi hiyo?
Jibu: Sikuanza na udiwani. Nilikuwa kiongozi kwenye kikundi cha watu wanaotoka Mkoa wa Mara wanaoishi Mererani. Tulikuwa tunasaidiana katika shida na raha.
Umoja wetu huu wa Mara Group ulituweka pamoja na kuwa mfano wa kuigwa na watu wa jamii nyingine ya eneo lile kiasi cha watu kuonyesha kuvutiwa nasi.
Wakaniomba nigombee uongozi kwa nafasi ya udiwani ili niweze kuwaunganisha wananchi wa eneo lile kwa ujumla wao, kama nilivyofanya kwa jamii ile ya watu wa Mara.
Nilichaguliwa kuwa diwani mwaka 2010 na mimi nikaanza kuwatumikia wananchi wa kata ile kusimamia na nikafanikisha maendeleo kwa kiasi kikubwa.
Wakati wa kampeni zangu, sikuomba ubosi kwao niliomba utumishi, ndiyo sababu ya mafanikio yangu, nimeweza kushirikiana nao katika mambo mengi ya kimaendeleo.
Swali:Katika kipindi chako cha uongozi unajivunia nini kukifanya kwa mafanikio?
Jibu: Katika kipindi changu cha uongozi tangu mwaka 2010 hadi sasa, nimeweza kusimamia miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto na sehemu ya kuhifadhia miili ya marehemu kwenye kituo cha afya na ujenzi wa nyumba ya watumishi iliyogharimu Sh30 milioni .
Pia nimeshiriki na kufanikisha ukarabati wa maabara ya kituo cha afya cha kata, ujenzi wa kilomita sita za barabara, makaravati ya barabara katika kata hii.
Vile vile nimeviwezesha vikundi vitano vya ufugaji kuku na pia kuwezesha ukarabati wa tanki la maji linalosambaza maji katika kata hii pamoja na kuwezesha kufanikisha kujenga sehemu ya mifugo kunywa maji.
Swali: Katika kazi zako za udiwani, unakabiliwa na changamoto zipi?
Jibu: Katika kazi yoyote hapakosi changamoto. Na katika uongozi changamoto ni pamoja na zile ambazo ni kero zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
Kwenye kata yangu zipo nyingi, baadhi ni ukosefu wa maji safi na salama, upungufu wa dawa katika kituo cha afya kutokana na kuhudumia wagonjwa wengi.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa walimu wa kutosha wa masomo ya sayansi na hisabati umesababisha kufeli kwa wanafunzi wengi, kutokuwa na jengo la ofisi ya kata na upungufu wa vyumba vya madarasa, madawati na matundu ya vyoo.
Swali: Una mikakati gani katika kukabiliana na changamoto zinazokukabili?
Jibu: Nina mikakati mingi lakini kikubwa ni kufanya kazi kwa ukaribu na watendaji wa halmashauri ya wilaya na kuwakumbusha wazingatie makubaliano yanayohusu elimu na afya kwa kuwa mpango huu ukifuatiliwa tatizo la maji litakwisha.
Ili kukamilisha utawala bora ni pamoja na kuwa na jengo la kata, hivyo halmashauri ya wilaya katika mpango wake wa kujenga ofisi ya kata kwa kila kata, tunaomba tupatiwe kipaumbele, hiyo ni kutokana na wingi wa watu wanaotaka huduma za kiofisi.
Swali: Ni jambo gani ukiliangalia unajivunia kulifanikisha?
Jibu: Mafanikio makubwa ninayojivunia ni hamasa niliyoitoa kwa wananchi wa kata hii kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili watibiwe mwaka mzima kwa kutoa Sh10,000 kila kaya yenye baba, mama na watoto wanne pindi wakipata ugonjwa.
Nilianza kwa kujitolea kuwalipia watu wasio na uwezo Sh500,000, kaya 50 sawa na watu 300 kwenye kata hii, ambapo kila kitongoji nimesaidia kaya 10. Mpango huu ulifanikiwa na sasa hakuna tatizo la matibabu kwani wananchi wangu wanatibiwa kwa CHF.
Vile vile niliwahi kutoa fedha zangu Sh 5 milioni kwa ajili ya kuvuta maji hadi Shule ya Msingi Endiamtu.
Kwa sasa shule hiyo inatumia maji hayo, hivyo kwa sasa wanafunzi na walimu wananufaika na huduma hiyo muhimu.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa