Home » » UTEUZI WA SUMAYE HANANG GUMZO

UTEUZI WA SUMAYE HANANG GUMZO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SHEREHE za kumsimika Waziri Mkuu, mstaafu Fredrick Sumaye, aliyechaguliwa kuwa Kamanda wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Hanang, zimeota mbawa.
Sherehe hizo zilizopangwa kufanyika Oktoba 18, zimeahirishwa katika mazingira yanayotajwa ni rafu za kumuumiza Sumaye anayetajwa kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Uteuzi huo wa Sumaye, ulizua gumzo mkoani Manyara kwa kuwa baadhi ya makada walitarajia nafasi hiyo iende kwa Mbunge wa Hanang, Mary Nagu.
Mmoja wa kada wa CCM kutoka Manyara, amelalamikia ukiukwaji haki unaoanzia ngazi ya sekretarieti ya chama kwa lengo la kumkwamisha Sumaye na baadhi ya wanachama.
Alisema baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya chama, kwa kile alichodai kutoa maelekezo na  kuwatisha baadhi ya viongozi wa chama ngazi za Wilaya ni mikoa kutowaunga mkono baadhi ya makada wa chama hicho ili kuvuruga mipango yao.
“Unasikia mwandishi, shughuli ya kumsimika Sumaye ilipangwa na Wilaya ifanyike Oktoba 18 mwaka huu na alijulishwa mapema, lakini wamesikia kuna mashinikizo kuzuia shughuli hiyo,” alilalamika kada huyo.
Alibainisha kuwa, uongozi wa Mkoa umesema wamepata maagizo kutoka ngazi za juu kwamba, Kamanda wa Vijana Mkoa asimikwe kwanza kabla ya Wilaya.
Alibainisha kuwa kiutaratibu, makamanda wa Wilaya ndio huwa wa kwanza kusimikwa na yule wa Mkoa anakuwa wa mwisho.
Hata kwenye chaguzi za chama chetu, tunaanzia kwanza ngazi ya matawi hadi taifa, iweje leo kwa hili tuanzie juu kwenda chini?”Alihoji.
Kada huyo, alilalamika na kudai kwamba mazingira yanayojitokea katika suala hilo ni sawa na yaliyojiri wakati wa kinyang’anyiro cha  kugombea kiti cha mjumbe wa NEC Wilayani humo.
Alisema katika uchaguzi huo, Sumaye alilalamika kutotendewa haki na kulifikisha suala hilo hadi ngazi za juu za chama huku akiweka bayana kwamba, uchaguzi huo uligubikwa na rushwa.
Tanzania Daima, lilimtafuta Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Regina Ndege, kutoa ufafanuzi wa jambo hilo lakini simu yake ilikuwa haina majibu wakati wote.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda kujua utaratibu wa kuwasimika makamanda wao, ambako alisema si lazima asimikwe Kamanda wa Mkoa ndiyo wasimikwe wa Wilaya.
Alisema kilichotokea Hanang ni kuwa Kamanda wa Mkoa, Christopher Ole Sendeka aliteuliwa Desemba mwaka jana lakini mpaka sasa hajasimikwa kutokana na muingiliano wa shughuli na si mizengwe kama inavyodaiwa.
Alibainisha kuwa Sumaye aliteuliwa Juni mwaka huu na inavyoonekana Wilaya wamewahi kufanya maandalizi ya kumsimika ndiyo maana wanalalamika wanaposikia wanapaswa wasubiri zaidi.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa