CHAMA Cha Walimu Nchini (CWT), wilayani Ngorongoro kimemlalamikia
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, John Mgalula kwa kukataa
kuunda Baraza la Wafanyakazi.
Imedaiwa kuwa hali hiyo imepunguza ari ya watumishi wa halmashauri
kufanya kazi hasa walimu jambo linalochangia shule za wilaya hiyo
kufanya vibaya kitaaluma.
Hayo yalisemwa juzi na Katibu wa CWT wilayani hapa, Emanuel Ledio alipozungumza na Tanzania Daima kuhusu kero ya muda mrefu.
Alisema CWT ilimuandikia barua mara mbili, wamekutana na mkurugenzi
huyo ofisini kwake mara mbili wakimuhimizi kuunda chombo hicho kisheria
lakini amegoma.
“Hilo ndiyo jukwaa pekee la wafanyakazi kueleza dukuduku zao ili
kuboresha utendaji kazi, hapa mnaweza kutengeneza mkataba wa hali bora
kazini lakini mkurugenzi huyu hataki kuunda na haelezi sababu za yeye
kutounda baraza hilo,” alisema Ledio.
Alitaja kero wanazokumbana nazo walimu wa Ngorongoro kuwa ni kwenda
kilomita 200 kufuata mishahara yao wilayani Karatu na wakati mwingine
hulazimika kulala huko kutokana na shida ya usafiri.
Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu, Mgalula alikana kupata
barua na kukutana nao kuhusu jambo hilo hivyo aliwataka wafike ofisini
kwake.
“Wamekuja kulalamika kwako mbali kiasi hicho? Kwa nini wasije ofisini
kwangu tuongee uso kwa uso? Sasa kwa kuwa wameamua kukufuata basi
waambie waje ofisini kwangu Jumatatu asubuhi na wajitambulishe kuwa wao
ndio waliokuja kwenye ofisi za magazeti tutayazungumza na hilo baraza
tutaliunda,” alisema mkurugenzi huyo.
chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment